NHIF YABORESHA ULIPAJI WA MADAI, YASHUSHA MUDA HADI SIKU 50
Na Mwandishi wetu-Dar es salaam
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Dkt.Irene Isaka,amesema mfuko huo umepunguza muda wa wastani wa kulipa madai ya vituo vya kutolea huduma za afya kutoka siku 120 hadi 50, hatua inayolenga kuongeza ufanisi wa huduma na kuimarisha ushirikiano na watoa huduma.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa NHIF pia amesema kuwa mafanikio hayo ni sehemu ya maboresho yaliyofanyika katika kipindi cha miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Mfuko huo, yakihusisha usimamizi wa rasilimali, udhibiti wa matumizi na kuimarisha mifumo ya utoaji huduma.
Hayo ameyasema Novemba 6,2026 Jijini Dar es wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari nakubainisha kwamba mapato ya Mfuko yameongezeka kwa asilimia 10.3, huku matumizi yakipungua kwa asilimia 10.
Amesema hali hiyo imesaidia kushusha uwiano wa gharama za matibabu dhidi ya mapato kutoka asilimia 87 hadi 71, karibu na kiwango cha asilimia 70 kinachotajwa kimataifa kwa uimara wa mifuko ya bima ya afya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, ameipongeza NHIF kwa kutambua mchango wa wanahabari katika kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa bima ya afya.
Balile amesema nafasi 100 za bima zilizotolewa kwa wanahabari ni fursa muhimu na ameahidi TEF kushirikiana na Mfuko kubaini waandishi na wahariri wanaohitaji huduma hiyo ili wapatiwe kwa haraka zaidi.
Halikadhalika Mratibu wa Elimu kuhusu Bima ya Afya kwa Wote kutoka Wizara ya Afya, Said Makora,amesema Serikali inaendelea kuongeza watumishi wa afya ili kukidhi mahitaji yanayotarajiwa kuongezeka kutokana na utekelezaji wa mpango wa bima ya afya kwa wote.
Hata hivyo kati ya ajira 5,000 zilizotolewa katika sekta hiyo, watumishi 808 wamepelekwa katika ngazi ya huduma za afya ya msingi, huku jitihada zikiendelea kukabiliana na upungufu wa wataalamu, hususan katika huduma za mama na mtoto na matibabu ya saratani.



