RC MABULA ATAKA KASI MPYA YA MAENDELEO TABORA

 



Na Allan Kitwe, Tabora


MKUU wa Mkoa wa Tabora Dkt Angeline Mabula amepokelewa rasmi katika Mkoa huo na kueleza wazi kuwa anataka kuona Mkoa huo ukipiga hatua kubwa zaidi kimaendeleo na kila mtumishi kutimiza wajibu wake ipasavyo.


Ameeleza hayo jana alipokuwa akiongea na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Taasisi, Sekretarieti ya Mkoa, Wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Makatibu Tawala wa Wilaya na Maafisa Tarafa.


Amesema kuwa Mkoa huo ni miongoni mwa Mikoa yenye fursa nyingi za kiuchumi, lakini utekelezaji wake hauridhishi licha ya jitihada zinazofanyika, hivyo akasisitiza kuwa anataka kuona Tabora ikienda kwa kasi zaidi.


Ametaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni maeneo ya uwekezaji viwanda, bwawa la Wembele, eneo la ujenzi wa Bandari Kavu, Ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo unaoendelea sasa na nyinginezo.




‘Najua baadhi ya mipango utekelezaji unaendelea, ila kasi yake hairidhishi, na hili ndilo nalotaka lifanyike, nataka Tabora iende kwa kasi kubwa zaidi, na kila mmoja asimame kwenye zamu yake’, ameongeza.


Dkt Mabula amesisitiza kuwa watumishi wote kuanzia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa hadi Wilayani wanatakiwa kufanya kazi kwa nidhamu kubwa na mshikamano, na kila mmoja atimize wajibu wake ipasavyo.


‘Tutumie muda wetu vizuri kwa kufanya kazi inayotakiwa na sio kuendekeza malumbano au majungu, tukosoane vizuri ili kujenga na kudumisha ushirikiano wetu, sitapokea majungu yoyote ofisini kwangu’, amedokeza.


RC Mabula ameeleza kuwa Ofisi yake ipo kwa ajili ya wananchi, hakuna haja ya ‘appoitment’, na kuonya kuwa mwananchi atakayeleta malalamiko ya kutosaidiwa na Mtumishi yeyote wakiwemo Wakuu wa Wilaya, ataeleza kwa nini hakumsaidia.


Aidha ameagiza fedha zote zinazoletwa na Serikali au Wadau wa Maendeleo kwa ajili ya shughuli za maendeleo zisimamiwe ipasavyo na taarifa ya matumizi yake ipatikane wakati wote na kazi iliyofanyika ionekane, kinyume na hapo, itakula kwao.


Awali akimkaribisha, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dkt John Mboya ameeleza kuwa serikali kuu imeleta zaidi ya shilingi bilioni 96 za maendeleo katika Mkoa huo, ambapo bil 8.2 ni kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na bil 88.8 za halmashauri.


Mwisho

Powered by Blogger.