RHINO RANGERS WAMWAGIWA MAMILIONI YA FEDHA
Na Allan Kitwe, Tabora
TIMU ya Rhino Rangers FC ya Mkoani Tabora inayoshiriki Ligi ya Championship imeungwa mkono na wakazi wa Mkoa huo kwa kuchangiwa zaidi ya sh mil 200 ili kuiwezesha kufanya vizuri katika ligi hiyo na kupanda ligi kuu.
Kiasi hicho ambacho ni fedha taslimu na ahadi kimepatikana kwenye harambee maalumu iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Dkt Angelina Mabula iliyofanyika jana katika ukumbi wa ‘Muungano Mess’ Mjini hapa, na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali.
Dkt Angelina Mabula ameeleza kuwa timu hiyo ni ya wana Tabora na imebeba alama ya Mkoa, hivyo akaomba viongozi, wafanyabiashara, wakulima, wafanyakazi, na wakazi wote wa Mkoa huo kuiunga mkono kwa hali na mali.
Amewataka kutosikiliza uongo na maneno ya mitaani kuwa timu hiyo inauzwa, na kusisitiza kuwa timu hii ni ya wana Tabora, itaendelea kuwepo Tabora, hivyo akawataka kupuuza maneno hayo na kueleza wazi kuwa ‘HAIUZWI’.
‘Mimi ndio mlezi wa timu hii, naomba wapenzi wa michezo na wana Tabora wote tuiunge mkono, na kuipa kila aina ya msaada ili vijana wetu waweze kupata mahitaji yao yote ikiwemo posho ili wacheze kwa moyo na ari kubwa’, amesema.
Awali Mwenyekiti wa klabu hiyo Kanali William Joshua Lovukenya amemweleza Mkuu wa Mkoa kuwa timu hiyo ni ya wananchi wote, sio ya jeshi, na jina la Rhino (faru) limebeba alama ya nyara za serikali zilizopo nchini.
‘Nawashukuru sana Viongozi wa chama na serikali, wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, watumishi,wakulima, machinga, bodaboda na mamalishe kwa kuendelea kuiunga mkono hadi hapo ilipofikia, sasa tunataka ipande ligi kuu’, amedokeza.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora Said Nkumba na MNEC wa Mkoa huo Mohamed Nassoro Hamdan wamempongeza Mkuu wa Mkoa kwa kukubali kuwa mlezi wa timu hiyo na dhamira yake njema ya kuona timu hiyo inapanda ligi kuu.
Wameahidi kumuunga mkono na kumpa ushirikiano wa dhati ili kuhakikisha dhamira yake ya kuona Mkoa huo unakuwa na timu ya ligi kuu inatimia.
Mwisho


