TISEZA YASAJILI MIRADI 1,148 YA UWEKEZAJI YA THAMANI DOLA ZA KIMATEKANI BILIONI 15.32
Na Mwandishi wetu-,Dar es salaam
MAMLAKA ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imesajili miradi 1,148 ya uwekezaji yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 15.32, inayotarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 344,031.
Akizungumza leo Novemba 2, 2026 katika kikao kazi kati ya mamlaka hiyo, wahariri na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri amesema kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Septemba 2026, mamlaka hiyo imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi, kuboresha huduma kwa wawekezaji na kuendeleza Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZs).
TISEZA ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Na. 6 ya mwaka 2025, kwa kuunganisha iliyokuwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Kukuza Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA).
Amesema kuwa mamlaka hiyo ina jukumu la kuratibu, kukuza na kuwezesha uwekezaji, kusimamia uendelezaji wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi pamoja na kuishauri Serikali kuhusu masuala ya uwekezaji na kuboresha mazingira ya biashara nchini.
Amesema kuwa kati ya mtaji wa uwekezaji uliosajiliwa, uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ya nchi (FDI) ulifikia dola za Marekani bilioni 9.60, huku uwekezaji wa ndani ukifikia dola bilioni 5.72.
“Katika kuendeleza Maeneo Maalum ya Kiuchumi, TISEZA imeelekeza nguvu zake katika maeneo ya Bagamoyo, Kwala na Nala kwa lengo la kuvutia wawekezaji katika sekta za viwanda, uzalishaji, uchakataji wa mazao, biashara na usafirishaji.
“Kupitia juhudi hizo, mamlaka ilipokea maombi zaidi ya 80 ya matumizi ya ardhi katika maeneo hayo, ambapo maombi 43 yalifikia hatua ya kusainiwa kwa mikataba ya upangishaji au haki za upangaji wa ardhi. Uwekezaji unaotarajiwa katika maeneo hayo unakadiriwa kufikia zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.5 na kuzalisha ajira zaidi ya 15,844” amesema. Teri
Aidha amesema kuwa TISEZA imeendelea kuratibu ujenzi wa miundombinu katika eneo la Bagamoyo SEZ, ikiwemo barabara yenye urefu wa takribani kilomita 3.116, pamoja na kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha upatikanaji wa umeme katika eneo la hekta 151.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa katika eneo la Tanga SEZ, maandalizi ya Mpango Kabambe wa matumizi ya eneo hilo yamefikia asilimia 12.
Teri amesema kuwa katika kuboresha huduma kwa wawekezaji, TISEZA imeendelea kutumia Kituo cha Huduma za Pamoja kwa Wawekezaji (OSFC) na Kituo cha Huduma kwa Wawekezaji wa Kimkakati (PISC).
“Kupitia vituo hivyo, wawekezaji 524 walihudumiwa katika Premium Lounge. Kati yao, wawekezaji 34 walifanikiwa kusajili kampuni, huku miradi 83 ikisajiliwa kupitia mifumo ya Certificate of Incentives na Export Processing Zones (EPZ).
“Vilevile, wawekezaji 142 walipata ushauri kuhusu masuala ya ardhi, kodi, fursa za uwekezaji na huduma za kifedha” amesema Teri.
Amesema kuwa zaidi ya wajumbe 107 kutoka nchi na maeneo mbalimbali, yakiwemo Afrika, China, Japan, Ulaya, Urusi na Bulgaria, walipatiwa ushauri kuhusu fursa za uwekezaji nchini.
Pia, mamlaka imeandaa na kuzindua Sera ya Watoa Huduma kwa Wawekezaji ya mwaka 2025 (Investor Service Providers Policy, 2025), pamoja na jukwaa la watoa huduma hao kwa lengo la kuweka utaratibu wa usajili, ada na utoaji wa huduma kwa wawekezaji kwa uwazi na ufanisi

