HATUKOPI KWA KUWEKA REHANI RASILIMALI ZETU; MKUMBO

Na Mwandishi Wetu, Dar


Waziri wa Mipango na Uwekezaji Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa mkopo wa dola Bilioni 2.5 ambazo Tanzania imeupata kutoka Korea hauna masharti yoyote yale ya kuweka rehani rasilimali za Tanzania kama inavyosambazwa na mitandao ya kijamii.

Waziri Kitila amesema mkopo huo wala hauna masharti ya kutoa bahari na madini kwa wakorea kama inavyosambazwa bali amesema ni mkopo ambao una faida kubwa kwa nchi.

Ameyasema hayo leo Juni 6,2024 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu ziara rasmi ya Kiserikali aliyofanya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Jijini Seoul, Jamhuri ya Korea kuanzia Mei 31, 2024 hadi Juni 05, 2024.

Alisema mkopo huo walioupata si wa kwanza kupokea kutoka Korea na kusisitiza kuwa kukopa ni muhimu kwa sababu ni moja ya nyenzo za kujenga uchumi wa nchi, kujenga uwezo wa serikali kutoa huduma kwa wananchi wake.

"Huu siyo mkopo wa kwanza tunaupokea kutoka mataifa mbalimbali duniani, mmemsikia Waziri wa fedha akisema bungeni nchi yetu imeshakopa matrioni, na hakuna mkopo hata mmoja ambao tumewahi kupokea kwa maana ya kuweka rehani rasilimali yetu mojawapo hasa za asili, huu ni mkopo wa pili kupokea kutoka Korea tulikuwa tumekopa Bilioni 1,''alisema na kuongeza 

"Sisi kama nchi tumeshajiwekea utaratibu kwenye sera zetu za kifedha namba moja ni kutumia kadiri iwezekanavyo mapato ya ndani na ndio maana tunapambana kuongeza uwezo wa ndani kwa maana ya mapato kupitia kodi ya watanzania, kipaumbele cha Tanzania kuchukua mikopo yenye masharti nafuu, na kwaajili ya kujenga uwezo wa nchi,mkopo huu tutalipa kwa miaka 40 na riba yake ni asilimia 0.01 na utaanza kulipa  baada ya miaka 25 tangu tulipopokea,"alisema.  

Aidha alisema wanazingatia sheria zote za nchi katika mikopo hiyo na kwamba fedha hizo zinakwenda katika maeneo ambayo yana tija na kuongeza kuwa watu wakiona Rais amesafiri kwenda nchi mbalimbali ni kwa faida ya watanzania na nchi kwa ujumla.

Prof. Kitila alisema  kipaumbele chao ni kuchukua mkopo wenye nafuu na kwenda kwenye sekta za uzalishaji hawakopi kwenda  kununua magari na kulipa mishahara,bali kufanya maendeleo ambapo mkopo ni wa miaka 40 na riba yake ni asilimia 0.01 na wanaanza kulipa mwaka wa 26 kama masharti ya mkopo inavyosema.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Dkt Natu El-Maamry Mwamba alisema baada ya kufanikiwa kupata mkopo wa fedha hizo dola Bilioni 2.5,wataanza kuhainisha miradi ambayo itaenda kuwasilishwa.

''Kwa kawaida tumekuwa tukipokea misaada kutoka Korea katika maeneo ya Nishati,Usafiri,Miundombinu ,Elimu,Afya,Kilimo na Maji kwahiyo mkopo huu unaweza  kwenda katika maeneo haya au zaidi,''alisema.

Dkt. Natu alisema kwa utaratibu kuna Tume ya Mipango nchini ambayo ndipo mipango itakapoanzia ambapo hadi sasa tayari imeanza kuhainisha maeneo ya miradi hiyo na kupelekwa katika wizara ya fedha kisha  kuwakutanisha watu wa Korea na Tanzania kukaa kwa pamoja na kujadili ili kupata miradi ambayo itatekelezwa.

''Miradi hiyo itafata kipaumbele chetu na maeneo ambayo tunataka kujikita nayo kama kupata teknolojia ,kwa wiki inayofata tunapokea miradi tukae tuichambue na kukaa na kufanya policy Dialogue na wenzetu wa Korea waone,miradi yetu ni kipaumbele chetu sisi,''alisema.

''Tutakapokubaliana hiyo miradi ndo tunaenda katika kutekeleza baada ya kukaa kikao hicho na wenzetu,''alisisitiza

Powered by Blogger.