𝗡𝗖𝗛𝗜 𝗪𝗔𝗡𝗔𝗖𝗛𝗔𝗠𝗔 𝗭𝗜𝗡𝗔 𝗝𝗨𝗞𝗨𝗠𝗨 𝗟𝗔 𝗞𝗨𝗜𝗟𝗜𝗡𝗗𝗔 𝗝𝗨𝗠𝗨𝗜𝗬𝗔 𝗬𝗔 𝗔𝗙𝗥𝗜𝗞𝗔 𝗠𝗔𝗦𝗛𝗔𝗥𝗜𝗞𝗜 - 𝗪𝗔𝗭𝗜𝗥𝗜 𝗠𝗔𝗞𝗔𝗠𝗕𝗔


Na Mwandishi wetu 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Januari Makamba amesema nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zina jukumu kubwa la kuilinda jumuiya hiyo.

Mhe. Makamba amesema hayo alipozungumza katika Mkutano wa faragha wa siku tatu wa mashauriano ya kisiasa wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki wanaokutana mjini Zanzibar.


“Madhumuni ya mkutano huu ni kuifanya Jumuiya yetu kuwa imara na yenye nguvu, jukumu letu kubwa na la msingi ni kuwa na umoja wenye nguvu, tumeona katika siku za nyuma ambapo tulipojaribu kuwa na umoja huu lakini ukavunjika, madhara ya kuvunjika kwa umoja ule bado tunayo na kwa hali hiyo hatupaswi kurudia tena makosa hayo,” alisema Mhe. Makamba.

Amesema mkataba wa uanzishwaji wa Jumuiva unaeleza kuwepo kwa umoja bora kabisa ambao utapelekea katika umoja wa kisiasa na kuelekea katika umoja huo imara ndio mafanikio ya Jumuiya na kuzisihi chi wanachama kuhakikisha zinafikia mafanikio hayo.


Amesema nchi wanachama zinajua kuwa kufikia mafanikio hayo kuna milima, mito na mabonde ya kuvuka na kwamba ni lazima kuvuka vikwazo hivyo ili kuiwezesha Jumuiya kufikia malengo ya kuanzishwa kwake.

Wakizungumza katika mkutano huo Mawaziri kutoka nchi wanachama wa EAC wanaohudhuria mkutano huo wameipongeza Tanzania kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kwanza na wa kihistoria kufanyika ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mkutano huo wa faragha unajadili taarifa ya Mwenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya; hali ya amani, usalama, siasa na uhusiano kati ya nchi wanachama; kutathmini na kujadili mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na masuala yanayokwamisha ufikiwaji wa malengo ya programu na miradi inayopangwa.

Mkutano kazi huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 07 Mei, 2024.


Powered by Blogger.