CDF JENERALI JACOB JOHN MKUNDA APOKEA UJUMBE WA JESHI LA CHINA
Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
Ujumbe wa Makamanda walioongozana na meli ya matibabu kutoka Jeshi la Ukombozi la Watu wa China umemtembelea Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi(CDF) Jenerali Jacob John Mkunda ofisini kwake Upanga jijini Dar es Salaam na kufanya mazungumzo naye.
Katika mazungumzo hayo Kiongozi wa Ujumbe huo, Rear Admiral HongBo Ying amelishukuru Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa mapokezi makubwa pamoja na ushirikiano walioupata tangu walipowasili hapa nchini Julai 16, mwaka huu wakiwa na Meli Vita ya Matibabu.
Naye Jenerali Mkunda amesema JWTZ linapoelekea kuadhimisha kilele cha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake, linashirikiana na Jeshi la China katika kutoa huduma ya matibabu na mazoezi ya medani.
Aidha amewasihi watanzania kujitokeza kwa wingi kwenye tiba ili kupimwa afya zao pamoja na kupata matibabu bila malipo kwani JWTZ limeamua kushirikiana na Jeshi la China ikiwa ni muendelezo wa ushirikiano kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 60 ya JWTZ.
Matibabu hayo bila malipo yataanza rasmi Julai 18, mpaka 23, mwaka huu.
Tangu kuanzishwa kwa JWTZ miaka 60 iliyopita jeshi limekuwa na ushirikiano wa kidugu na Jeshi la China baada ya kuasisiwa na Marais wa kwanza wa nchi hizi mbili Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mao Zedong.
Mwisho