DKT.SAMIA AELEZA YALIYOJIRI KWENYE ZIARA YAKE KATAVI

 

Kutoka ukurasa wa X wa Rais SSH

"Jumapili njema mkoani Katavi ambako pamoja na mambo mengine, tumekuwa na mambo matatu makubwa muhimu kwa mkoa huu na nchi yetu kwa ujumla.

Moja, uzinduzi wa Jengo la Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi. Mkoa huu ni moja ya mikoa muhimu kiusalama kwa nchi yetu na lango la wageni toka nchi mbalimbali kusambaa mikoa mingine ya Tanzania, hivyo basi ubora wa miundombinu ya vyombo vya ulinzi na usalama mahali hapa ni moja ya jukumu letu kubwa kama nchi.


Mbili, uzinduzi na kuanza kutumika rasmi kwa maghala na vihenge vya kuhifadhia nafaka ambavyo vimejengwa na Serikali. Uwekezaji huu sasa unakuza uwezo wa Mkoa wa Katavi kuhifadhi nafaka toka tani 5,000 hadi 28,000 hatua ambayo inazidi kuwapa wakulima uhakika wa kilimo chao kibiashara na uhakika wa chakula kwa nchi yetu.


Tatu, nimetazama na kuridhishwa na kazi nzuri ya maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi. Huduma ambazo miaka michache iliyopita wananchi walizifuata Dar es Salaam na Mwanza, sasa wanazipata karibu zaidi ikiwemo vifaa na wataalamu. Ujenzi wa hospitali hii una hatua tatu; tumemaliza hatua ya kwanza, na nimewahakikishia kuwa tayari tumewatengea fedha za hatua ya pili ili waendelee na kazi."


Powered by Blogger.