Gen Z ni kizazi gani?
NAIROBI: Kenya imeshuhudia maandamano siku za hivi karibuni yaliyokuwa yakishinikiza kuondolewa kwa Muswada wa Fedha 2024, uliopendekeza ushuru zaidi ili kufadhili bajeti ya mwaka mpya wa kifedha.
Licha ya kuwa sio maandamano ya kwanza nchini humo, yalivutia kiasi kikubwa cha vijana wa kizazi cha Z maarufu kama Gen Z, waliojitokeza barabarani katika maeneo tofauti tofauti na kutumia zaidi teknolojia kupaza sauti zao.
Kuna sintofahamu kuhusu ni lini kizazi cha Gen Z kinaanza na kumalizika lakini kinaundwa na watu waliozaliwa kati ya miaka ya 1990 na katikati ya miaka ya 2000.
Gen Z wameanza kutumia intaneti tangu wakiwa na umri mdogo, ikiwa sio maisha yao yote, na inafurahia teknolojia na mitandao ya kijamii.
Kwa hakika, kizazi hiki kilizaliwa kabisa ndani ya enzi ya kiteknolojia na kinafahamu vyema ulimwengu wa teknolojia na utandawazi.
Hayo yamejidhihirishwa wakati wa maandano ya nchini Kenya, walipoonekana kutumia mitandao kujipanga na kutekeleza walichotaka kifahamike na jamii kwa ujumla.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Calvin Muga anasema kuwa matumizi ya mitandao ya kijamii na intaneti yalikuwa chombo muhimu sana cha kupashana habari kabla, wakati wa maandamano hayo.
‘Wengi wao wana uzoefu na ni watumizi wakubwa wa mitandao ya kijamii na hili lilirahisisha sana wao kuwasiliana na kupanga maandamano yaliyofanyika,’ anasema Muga.
Kwa hivyo, kizazi cha Gen Z kina nia iliyo wazi zaidi kuliko vizazi vilivyotangulia na ifahamike kuwa mitindo na mawasiliano yao yanashirikishwa kote ulimwenguni.
BBC Swahili imezungumza na Patience Mwende Muia, mmoja wa vijana aliyezaliwa ndani ya kizazi cha Gen Z kufahamu zaidi jinsi kinavyotaka kuchukuliwa katika jamii.
Bi. Muia anakiri kuwa kizazi hiki kina sifa nzuri na mbaya.
"Kizazi hiki...ni watu ambao wanaelewa, wameona na hawapuuzi vitu. Pia ni kizazi ambacho kinapenda vitu kulingana na teknolojia na ubunifu. Kile ambacho watu wanasema ni kibaya kwetu, ni kwamba tuna msimamo...hatutingishiki"
Chanzo: BBC Swahili