"NAMTABIRIA RAIS SAMIA USHINDI WA KISHINDO 2025"-ASKOFU MWANKEMWA



 < Ahimiza utunzaji Amani

<Asisitiza waumini kujiandikisha daftari la wapiga kura

Na Mwandishi Wetu

DAR ES SALAAM: Askofu wa kanisa la Uponyaji na Uzima, Zakayo Mwankemwa amewataka wananchi na waumini wa kanisa hilo kwa ujumla kuepukana na uovu.

Askofu Mwamkemwa aliyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akiwahubiria waumini wa kanisa hilo lenye makao yake makuu Segerea, Dar es Salaam baada ya kurejea kutoka mlimani alikokuwa kwa maombi ya siku 30.

"Nikiwa kama kiongozi wa kiroho wa ngazi ya juu katika kanisa hili, nasikitishwa sana na umomonyokaji wa maadili unaoendelea nchini hususan unaohusishwa na imani za kishirikina, ninalaani vikali mpango huu ovu unaoratibiwa na wafuasi wa shetani," alisema Askofu Mwankemwa.

Aidha, Mwankemwa aliwataka waumini na taifa kwa ujumla kulinda na kuitunza amani iliyopo nchini , iliyoasisiwa na viongozi wa Taifa hili, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume.

"Tukichezea amani iliyopo, itakuwa vigumu sana kuirejesha; mfano mzuri ni mataifa ya Magharibi na Mashariki ya Mbali yanavyohaha kujinasua ili ipatikane amani ya kweli lakini inashindikana.

Vile vile Askofu Mwankemwa aliwataka waumini na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura ambalo litawafanya waweze kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.

"Hamna budi kushiriki katika chaguzi mbalimbali, lakini niwasihi sana mjitokeze zaidi katika uboreshaji wa daftari la wapiga kura kwa kufanya hivyo, mtakuwa mmemuunga mkono Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan na serikali yake." alisema.

Akizungumzia mahusiano ya kanisa hilo na serikali Askofu Mwamkemwa alisema, yapo mahusiano mazuri sana na serikali na kwamba huiombea pamoja na viongozi wenye mamlaka akiwemo Rais Samia.

Hata hivyo, Askofu Mwankemwa amemtabiria Rais Samia ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao kutokana na namna anavyoendesha nchi kwa haki na demokrasia.

"Nimhakikishie Rais kuwa, uchaguzi wa mwakani atashinda kwa kishindo pamoja na chama chake(CCM), lakini pia nimuombe Rais wetu mpendwa aitishe mikutano ya mara kwa mara na viongozi wa dini zote kwa ajili ya kujadili maslahi mapana ya taifa na mustabali wake," alisema mbele ya waumini wake.

Kwa upande wake, Katibu wa Kanisa hilo Peter Masawe alisema kanisa hilo lenye miaka mitano tangu kuanzishwa kwake, limekuwa kimbilio la wenye dhiki na hitaji la kiroho.

"Hatujaanza muda mrefu lakini ashukuriwe Mungu , tumepata mapokeo mazuri kutoka kwa waumini ambapo kila uchao tunapokea waumini wapya wanaotaka kujiunga na Kanisa hili, hivyo, ni matarajio yetu kwamba huduma hii itaenea Tanzania nzima kwa uweza na utukufu wa Mungu , ambapo kwa sasa tuna makanisa mawili likiwemo hili la Tabata Makao makuu na Mbagala lakini baada ya miaka mitano tutakuwa tumefikia mikoa 15 Tanzania Bara na Zanzibar," alisema Peter.


Powered by Blogger.