"JIFUNZENI KUISHI MISINGI YA UONGOZI KWA VITENDO" -KAWAIDA AWAAMBIA UVCCM


 Na Mwandishi wetu

IRINGA: MWENYEKITI  wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Taifa (UVCCM) Mohammed Ali Kawaida , amewasihi Viongozi wa UVCCM Mikoa na Wilaya zote nchini,  kujifunza namna ya  kuishi kwenye misingi ya uongozi kwa vitendo huku wakizingatia Katiba, Kanuni na Miongozo ya Chama Cha Mapinduzi. 

Pia amewataka viongozi hao, kuhamasisha ushiriki wa vijana kikamilifu katika uandikishaji katika Daftari la kudumu la wapiga kura linazotazamiwa kufungiliwa rasmi Julai  20, 2024 Mkoani Kigoma.

Kawaida ameyasema hayo alipokua anahutubia Viongozi na Watendaji hao  katika Ufungaji wa mafunzo ya Viongozi na Watendaji wa UVCCM Mikoa na Wilaya zote nchi nzima yaliyofanyika  Chuo chua Ihemi Mkoani Iringa kuanzia Julai11  hadi 17,2024.

 Alisema mafunzo hayo waliyoyapata yanastahili hivyo yataenda kurahisisha utendaji kazi wao  katika maeneo yao ya kazi.


" Niwasihi sana nendeni mkaishi katika misingi ya Uongozi kwa kuzingatia Katiba, Kanuni na Miongozo ya Chama chetu,"alisema na kuongeza 

"Nimefurahishwa sana namna ambavyo mmekua wasikivu, mmeishi kwa ushirikiano, mmeishi kwa umoja na kuwa na nidhamu ya hali ya juu katika kipindi chote cha mafunzo yenu, mmedhihirisha kuwa ninyi ni Viongozi wa kweli na mmekua katika misingi ya uongozi ndani ya CCM,"alisema Mwenyekiti Kawaida.

Aidha aliwasisitiza kudumisha ushirikiano wa viongozi wa umoja wa Vijana wa CCM na Viongozi wa Serikali katika utekelezaji wa majukumu  katika maeneo yao.


"Ndugu viongozi niwasihi sana twendeni tukafanye kazi kwa ushirikiano sisi kwa sisi na tupendane mpaka watu waliopo nje washangae, lakini pia tushirikiane na viongozi wa serikali katika utekelezaji wa majukumu yetu kwenye maeneo yetu,"alisema.

Kawaida alisema ni vema viongozi hao wakafatilia  utekelezaji wa Ilani ya Chama  na kutangaza kazi nzuri zinazofanywa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika maeneo yao.


Akizungumzia Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. 

Alisema viongozi lazima wawe mstari wa mbele katika kuhamasisha vijana waweze kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa,vijiji na vitongoji  2024 na uchaguzi mkuu 2025.

"Sisi viongozi lazima tuwe mstari wa mbele katika Uhamasishaji wa Vijana kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025, twendeni tukawape hamasa ya kutosha vijana kujiandikisha kwenye Daftari la kudumu la wapiga kura na kushiriki kikamilifu katika chaguzi zote",alisema.

Mafunzo hayo yamefungwa na Mwenyekiti  Kawaida,Ihemi Mkoani Iringa ambapo awali yalifunguliwa na  Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Balozi Dkt Emmanuel John Nchimbi  Julai 11,2024

Powered by Blogger.