TANZANIA , KOREA KUSINI ZAJADILI FURSA ZA UWEKEZAJI MADINI YA LITHIUM
DODOMA: Ujumbe wa Wataalam kutoka nchi ya Korea Kusini leo tarehe 19 Julai, 2024 umekutana na wataalam wa Wizara ya Madini Tanzania na kujadiliana kuhusu fursa za Uwekezaji zilizopo katika madini mkakati aina ya Lithium yanayo patikana nchini.
Akielezea kuhusu uendelezaji mikakati yaliyopo Tanzania Kamishna wa Dkt. AbdulRahman Mwanga amesema kuwa kwasasa suala la uchakataji na uongezaji thamani madini lipo kisheria hivyo kuja na mpango wa kuongeza thamani madini ndani ya nchi ni jambo zuri kwa maslahi ya Taifa.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Sonokonog ya nchini Korea Kusini Bw. Soo Hyun Byun amesema Kampuni hiyo iko tayari kufanya uwekezaji katika madini mkakati aina ya Lithium kuanzia hatua ya uchimbaji mpaka uongezaji thamani kabla ya kusafirisha nje ya nchi.
Bw. Byun amesema kupitia uwekezaji huo, zitakuwepo na fursa mbalimbali kama vile ujenzi wa miundombinu kuelekea eneo la mradi , ubadilishanaji wa teknolojia pamoja na kufungua wigo mpana wa uwekezaji na masoko wa malighafi zitokanazo na rasilimali madini.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Bw. Fredrick Mangasini amesema STAMICO ipo tayari kuingia mkataba wa makubaliano na Kampuni ya Sonokong kwa lengo kuongeza uwekezaji katika madini mkakati hususan kwa madini ya Lithium ambayo hivi sasa yanathamani kubwa duniani katika sekta nzima ya sayansi na teknolojia
Mangasini amefafanua kuwa, STAMICO kwa kushirikiana na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ambao wana taarifa za utafiti wa madini watatoa ushirikiano mkubwa ili kufanikisha uwekezaji huo.
Katika majadiliano hayo, Tanzania imewakilishwa na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na Tume ya Madini.
Kampuni ya SonoKong ina makao yake makuu jijini Seoul, ilianzishwa mwaka 1974 nchini Korea ya Kusini, ni kampuni inayojishughulisha na utafiti , uchimbaji na uchakataji wa madini lithium Barani Afrika.
šø:W/Madini
Chanzo: Haki Ngowi -X