MUHIMBILI YAANZISHA HUDUMA YA MAMA KUJIFUNGUA AKIWA KWENYE JAKUZI ILI KUPUNGUZA MAUMIVU NA HAKUNA KUONGEZEWA NJIA

 


Na Mwandishiwetu, DAR ES SALAAM 

Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeanza kutoa huduma kwa kina mama kujifungua wakiwa kwenye jakuzi maalum la kujifungulia (water birth pool) linalosaidia kumpunguzia maumivu mama kabla na wakati wa kujifungua na kupunguza hatari ya mama kuchanika uke.

Hayo yamesemwa leo na Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Mohamed Janabi wakati akifungua mafunzo kwa wauguzi/wakunga, madaktari wa kina mama na madaktari wa watoto kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Upanga na Mloganzila, Dodoma RRH, na Lugalo wanaohudhuria mafunzo ya siku tano hospitalini hapo kuhusu huduma hiyo yanayotolewa na Bi. Barbara Harper ambaye ni Mkunga kutoka Water Birth International nchini Marekani.

Kupitia huduma hii, mama mjamzito anaingia kwenye jakuzi lenye maji ya uvuguvugu na mtoto anazaliwa ndani ya jakuzi na kumwezesha mtoto kupata damu yote kutoka kwenye kondo la nyuma na kamba kitovu hivyo kupunguza idadi ya watoto wanaozaliwa na upungufu wa damu, kupunguza hatari kwa watoto kuzaliwa wakiwa na changamoto ya upumuaji, kumpa mtoto virutubisho vyote vinavyobakia kwenye kamba kitovu.

Kwa upande wa mama, huduma hii humsaidia kupunguza hatari ya kuchanika wakati akijifungua, pia mama hataongezewa njia kwani maji pamoja na mkao anaotumia unamsaidia kulegeza misuli hivyo mtoto kutoka kwa urahisi. Mama anakuwa karibu na mtoto mara tu anapozaliwa, kutokuwa katika hali ya msongo hivyo kumpa raha mama na mtoto, kupunguza muda wa mama kuwepo katika hatua za kujifungua, kupunguza idadi ya kina mama wanaojifungua kwa upasuaji na kuzuia matumizi ya dawa za kuongeza uchungu.

Ni mojawapo ya huduma inayoongeza utu, staha na heshima, ni salama na imekua ikitumika nchi mbalimbali duniani na kuna tafiti nyingi zilizofanyika kuthibitisha ubora wa huduma hii.

Powered by Blogger.