UDOM YAJIPAMBANUA KUANGALIA MATATIZO YA KIJAMII
Na Penina Malundo,DAR ES SALAAM
MAKAMU Mkuu wa Chuo cha Dodoma (UDOM)upande wa Mipango na Utawala,Profesa Wineaster Anderson amesema chuo chao kinajipambanua kwa kuangalia matatizo ya jamii na kuona namna gani wanaweza kuzitatua hususan katika eneo la afya na teknolojia.
Akizungumza hayo jana katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu kama Sabasaba,Prof.Anderson amesema wamekuwa wakifanya tafiti mbalimbali ambazo zimekuwa zinaleta teknolojia mpya.
Amesema licha ya kuwepo kwa changamoto ya rasilimali fedha kweye tafiti lakini wanaendelea kujitahidi katika eneo hilo.
"Tafiti zetu zimejikita katika jamii ya Watanzania na kutatua matatizo yaliyoko katika jamii,bila tafiti huwezi kuja na tekolojia mpya, huwezi kuja na ubunifu wowote kwahiyo UDOM imeweza kujipambanua,” amesema.
Aidha amewataka wananchi kutembelea banda lao lililopo katika maonesho hayo ilikuweza kuona tafiti na teknolojia mbalimbali mpya ambazo wamekuja nazo.
"Mwaka huu tumekuja na bidhaa mpya kuwaonesha Watanzania kwa sababu mwaka jana tulikuwa na bidhaa tofauti, mwaka huu tumekuja na aina za mashine ambazo zinasaidia katika sekta ya samaki na wanafunzi kutengeneza ‘rockets’,"amesema.
Aidha,Prof.Wineaster amesema wanafunzi wa chuo chao wamekuwa wakifanya tafiti kwa kushirikiana na wanataaluma ili kutengeneza bidhaa zenye teknolojia mpya.
Mbali na hiyo amesema Chuo chao kinatarajia kuzindua kampasi mpya mkoani Njombe ambapo inatarajia kujikita zaidi katika maeneo ya misitu na Kilimo.