TMA: UTABIRI WA MVUA MSIMU WA VULI


 Dondoo muhimu za msimu wa mvua za Vuli kipindi cha Oktoba – Disemba, 2024

Taarifa hii inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua za Vuli kipindi cha Oktoba - Disemba 2024, ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbalimbali kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, usafirishaji (nchi kavu, kwenye maji na angani), mamlaka za miji, afya pamoja na menejimenti za maafa. Utabiri huu ni mahsusi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Nyanda za juu kaskazini mashariki, Pwani ya kaskazini, Ukanda wa Ziwa Viktoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma). Kwa muhtasari, mwelekeo huo na athari zake unaonesha kuwa:

a) Mvua za Vuli, 2024
i. Mvua zinatarajiwa kuwa za Chini ya Wastani hadi Wastani katika maeneo mengi na zinatarajiwa kuanza kwa kusuasua na kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha.
ii. Mvua za Vuli zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Septemba, 2024 katika ukanda wa Ziwa Victoria na kusambaa katika maeneo mengine katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Oktoba, 2024. Mvua zinatarajiwa kuisha wiki ya nne ya mwezi Disemba, 2024.
iii. Mvua za Vuli zinatarajiwa kuongezeka kidogo mwezi Disemba, 2024.
iv. Vipindi vya joto kali kuliko kawaida vinatarajiwa katika msimu wa Vuli.
v. Uwepo wa La-Niña hafifu unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika mvua za msimu wa Vuli, 2024.


b) Athari zinazotarajiwa
i. Upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi na hivyo kuathiri shughuli za kilimo.
ii. Kina cha maji katika mito na mabwawa vinatarajiwa kupungua.
iii. Kujitokeza kwa magonjwa ya mlipuko, kutokana na upungufu wa maji safi na salama.

Powered by Blogger.