MAFURIKO JANGWANI KUBAKI HISTORIA

 

Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. Zainab Katimba ametembelea eneo la Bonde la mto Msimbazi ambalo hivi karibuni Ofisi ya Rais TAMISEMi kwa kushirikiana na wizara ya Ujenzi kupitia TANROADS wanatarajia kusaini mkataba na mkandarasi wa ujenzi wa daraja la kimkakati la Jangwani jijini Dar Es Salaam.

Akiwa kwenye eneo hilo Mhe. Katimba amempongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwezesha mradi huo ambao ni suluhisho la mafuriko na kusimamisha shughuli za kiuchumi katika jiji la Dar Es Salaam.
“Huu ni uwekezaji mkubwa unaofanywa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwaajili ya kuhakikisha anatengeneza mazingira mazuri ya wakazi wa jiji la Dar Es Salaam na upekee wa mradi huu watu wote wanaostahili fidia tayari wamelipwa fidia zao” amesema

Mhe. Naibu Waziri Katimba amewataka watumishi wa kikundi kazi cha utekeleaji wa miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano kati ya benki ya Dunia na Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia TARURA kufanyakazi kwa ushirikiano na weledi katika Kutimiza majukumu yao ili kuhakikisha miradi inatekezwa kwa wakati na kwa umakini mkubwa.


Aidha, Mhe. Katimba amesema lengo kuu la mradi huu ni kukabiliana na mafuriko pamoja na kuimarisha mipango miji na uendelezaji wake katika eneo la chini la Bonde la msimbazi ambalo lina fursa kubwa za kiuchumi kwa jigrafia yake ya kuwa katikati ya jiji.

Gharama za mradi ikijuishwa ujenzi wa daraja,upanuzi wa mto na mawanda yake,ujenzi wa karakana ya BRT na fidia ya waathirika wa mradi zinakadiriwa kuwa dola milioni 260 sawa na shilingi bilioni 611 ambazo ni fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia(dola mil.200),Serikali ya Hispania (dola mil.30) na ruzuku kutoka Serikali ya Uholanzi (EURO mil.30).

Kwa upande wake Mratibu wa miradi ya ushirikiano kati ya Benki ya Dunia na Ofisi ya Rais TAMISEMI kupitia TARURA Mhandisi Humphrey Kanyenye amesema eneo hili lipo tayari kwa ujenzi na taratibu zote zimekamilika ikiwemo ulipaji wa fidia kwa waathirika wa ujenzi wa miundombinu hiyo.

“Ujenzi wa daraja utaanza hivi punde tunasubiri ratiba ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa daraja lakini daraja litakuwa na urefu wa mita 390 na litainuka juu kwa mita 13.5 ambayo itakuwa mita 6 kutoka sehemu ambayo magari yanapita kwasasa na kwa urefu huu maji yote yatakuwa yanapita chini ya daraja” Amesema Mhandisi Kanyenye

Powered by Blogger.