ULEGA: SEKTA YA KUKU MUHIMU USALAMA WA CHAKULA

 


Na Mwandishi wetu, DAR ES SALAAM 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi nchini,Abdallah Ulega amesema kuna  umuhimu wa sekta ya kuku nchini katika kufanikisha usalama wa chakula na ukuaji wa uchumi nchini.


Ameyasema hayo jana wakati wa mkutano wa Jukwaa  la Tasnia ya Kuku na Ndege wafugwao ambae Tanzania ni mwenyeji wa mkutano chini ya ufadhili wa Muungano wa Mapinduzi ya Kijani barani Afrika (AGRA).


Amesema dhamira ya serikali ya awamu ya sita imeendelea  kuunga mkono sekta hiyo kupitia miradi inayolenga vijana, ubunifu, na uendelevu.


Ulega amesema kuwa takwimu zinaonesha kuwa ifikapo 2030 kuku watachangia asalimia 41 ya protini na kuwa watafiti nchini washirikiane na Serikali wanapotoa matokeo ili kutoleta taharuki kwa jamii kupitia matokeo ya tafiti zao.


“ Hivi karibuni watafiti walifanya utafiti kwa kutumia sampuli chache juu ya ulishaji wa kuku wanaofugwa na akina mama na vijana tafiti ile ilileta taharuki, kupitia Jukwaa hili nitumie fursa hii kuwaambia watafiti washirikiane na Wizara ili kutotoa taarifa za taharuki kwa jamii na kuwa Serikali inaweza kudhibiti wafugaji wasiofuata taratibu hivyo tusiharibu jitihada zinazofanywa na kukuza tasnia hii,” amesema na kuongeza


“ Tunawaheshimu na kuthamini kazi zao ila tuone wanapofanya tafiti na kupeleka kwa jamii tuwe na mkakati wa pamoja wa kufikisha tafiti hizo kwa jamii,”amesema  Ulega.


Amesema mkutano huo ni matokeo ya  mkutano wa AGRA uliofanyika Dar es alaam na kuongozwa na  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo AGRA walielezwa juu ya kuipa kipaumbele sekta ya ufugaji wa kuku kwa kuwa nchini Tanzania familia nyingi zinafuga kuku.


“ Tunawashukuru AGRA na Food Alliance kwa kutukubalia na ndio maana leo jukwaa la kwanza limefanyika nchini Tanzania na kutoa fursa kwa wafugaji wetu kujifunza na kujenga mahusiano,” amesema Ulega.


Kwa Upande wake , Waziri Mkuu wa zamani wa Ethiopia na Mwenyekiti wa Bodi ya Muungano wa Mapinduzi ya Kijani barani Afrika (AGRA), Dkt. Hailemariam Dessalegn, amesema kuwa fursa muhimu zilizopo kupitia ufugaji wa kuku ni chanzo cha protini, soko la uhakika na ajira kwa vijana na kushiriki katika mnyororo wa thamani.

“Jukwaa hili linatoa fursa ya kujifunza faida na changamoto katika tasnia hii na kuongeza ushirikiano,Kukuza tasnia hii katika nchi yetu inahitaji majukwaa kama haya na inahitaji utayari  wa wadau mbalimbali kwa kuwa wana uwezo wa kuwekeza ili kukuza tasnia hii,” amesema na kuongeza 

“Tanzania ni kinara wa kuwa na njia shirikishi na ni imani yangu itaendelea hivi chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia ili kufikia ajenda ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), haswa dhamira ya kumaliza njaa na umasikini ifikapo 2030. Hakuna nchi inayoweza kufikia mafanikio haya peke yake hivyo sera ya ukanda, mafunzo na majadiliano na mawasiliano ni muhimu kufikia malengo,"amesema.

Naye Mkurugenzi wa Nchi wa AGRA Tanzania,Vianey Rweyendela, amesisitiza umuhimu wa sekta ya kuku kama sehemu ya mifumo ya chakula nchini.

" AGRA imekuwa ikifanya kazi kwa ukaribu na wadau kuendeleza sekta hii yenye ahadi kubwa katika kuboresha lishe, kuongeza mapato ya kaya, na kukuza uchumi wa taifa,"alisema. 



Powered by Blogger.