SUMSUNG C&T YAINGIA TANZANIA
KOREA: Kufuatia ziara ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoifanya nchini Korea Kusini mwezi Juni, 2024, na mazungumzo aliyoyafanya na makampuni makubwa ya Korea Kusini, kampuni ya Samsung C&T (Construction and Trade) imefanya uamuzi rasmi wa kuingia kuwekeza nchini Tanzania na kufungua ofisi yake ya kwanza barani Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ujumbe huo ulifikishwa kwa Mheshimiwa Rais na Rais wa Samsung C&T, Bwana Sechul Oh katika mazungumzo yaliyofanyika Ikulu, jana. Mheshimiwa Rais amewakaribisha na kuwahakikishia Tanzania iko tayari kwa uwekezaji wao, na utayari wa kuwapatia kila aina ya ushirikiano watakaouhitaji.
Samsung C&T ndio kampuni mwanzilishi wa Kundi la Makampuni ya Samsung (Samsung Group) iliyoanzishwa mwaka 1938 na ndio iliyozaa makampuni mengine ya Samsung ikiwemo Samsung Electronics.
Samsung C&T ina mtaji wa dola za kimarekani bilioni 45, na peke yake ilitengeneza faida ya dola za kimarekani bilioni 2.1 kwa mwaka 2023. Kampuni hiyo inawekeza na kuendeleza miradi katika nchi 44 duniani kwenye maeneo ya nishati, viwanda, miundombinu mikubwa, kemikali, na sekta ya huduma.