TPDC YAFAFANUZI UHABA WA GESI YA CNG
Na Mwandishi wetu,DAR ES SALAAM
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetoa ufafanuzi juu ya sababu ya kutokea kwa changamoto ya upatikanaji wa gesi ya CNG iliyotokea hivi karibuni kwa vyombo vya moto vinavyotumia nishati hiyokuwa ni hitilafu ya umeme kwenye kituo cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam Oktoba 3, 2024 Kaimu Mkurugenzi wa Bishara ya Mafuta na Gesi wa TPDC Emmanuel Gilbert aliesema, kutokea kwa chagamoto hiyo kulisababisha hali tete na mkanganyiko kwa watumiaji wa vyombo hivyo.
"Kilichotokea na kuleta tafrani juzi ni kwamba kulitokea tatizo la umeme kwenye kituo cha uwanja wa ndege kwa sababu kinahitaji umeme ili kiweze kugandamiza ile gesi," alisema Gilbert na kuongeza,
Alifafanua kuwa, tatizo hilo la umeme lilichukua saa 21 kurekebishwa kutokana na kwamba lilitokea usiku na kuja kutatuliwa usiku saa 3 nakueleza kuwa huduma hiyo kwa sasa imerudi.
Gilbert alisema kuwa hadi sasa kuna vituo vitatu tu vinavyotoa huduma hiyo ambavyo ni cha Ubungo, Tazara na hicho cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.
"Kwa sasa kumekuwa na mwitikio mkubwa wa matumizi ya nishati hiyo kwani makadirio ya magari yanayotumia gesi nchini ni takribani 4800 wakati vituo hivyo vitatu uwezo wake ni kujaza magari 1200 hadi 1500 kwa siku.
Alifafanua kuwa inapotokea hitilafu yoyote kwenye kituo lazima mtu akae kwenye foleni kwa kati ya masaa mawili hadi manne ili aweze kupata huduma kwani kituo kimoja kinapopata tatizo vinabaki viwili tu.
Hivyo alisema katika kukabiliana na changamoto ya kuwa na vituo vichache, TPDC ina haki binafsi ya kuwekeza kwenye miondombinu ya gesi kwenye magari.
Ambapo mwishoni mwa mwaka 2022 baada ya kuona hawawezi kulisha nchi nzima na kutoa huduma ya vituo waliamua kufungua milango kwa Sekta binafsi kuwekeza kwenye sekta hii.
Amesema hadi sasa wameshatoa idhini kwa kampuni 40 kuwekeza kwanye ujenzi wa vituo hivyo, hata hivyo amesema mwitikio wa utakelezaji wa miradi haujawa na kasi kubwa.
Aidha amesema kuwa kuna kampuni ambazo zipo kwenye mchakato wa kujenga vituo vingine na wanatarajia Juni mwakani wanaweza kuwa na vituo vingine 13 vipya tofauti na vitatu vilivyopo sasa.