TANZANIA, UFINI KUSHIRIKIANA TEKNOLOJIA ZA KISASA SEKTA YA MISITU


Na Mwandishi Wetu, Joensuun , Finland

Tanzania itapata fursa zaidi ya kuboresha sekta yake ya misitu inayochangia kwa sasa asilimia 4.2 ya Pato la Taifa (GDP), kufuatia utayari wa Serikali ya Finland (Ufini) na wadau wengine wa teknolojia nchini hapa kusaidiana katika nyanja za teknolojia za kisasa.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 9, 2024 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, mara baada ya kutembelea makampuni na vituo kadhaa vya teknolojia za misitu katika mji wa Joensuun hapa Ufini unaosifika kuwa kitovu cha sekta ya misitu nchini hapa.

“Tumetembelea makampuni makubwa duniani yaliyoko hapa kama Abounat, John Deere, Business Finland na Kitivo cha Teknolojia za Misitu cha Chuo Kikuu Finland kiitwacho East Finland University,” ameeleza Dkt. Abbasi.

Moja ya makampuni mengi ya teknolojia za misitu yaliyojikita katika mji huu ni kampuni ya John Deere inayoongoza duniani kwa kubuni, kutengeneza na kuuza mitambo mbalimbali ya kupandia, kukata na kuvuna mazao ya misitu hususani mbao na mazao yake ili kuipa thamani sekta hiyo kuwa ya kibiashara zaidi kutokana na uzoefu wa Finland.


Ufini ambayo imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali ya kusaidia sekta ya misitu nchini Tanzania ukiwemo Mradi wa Forvac uliomalizika hivi karibuni uliochagiza ajira 500,000 katika sekta hiyo, sasa iko tayari kusaidia mradi mwingine mpya kuendeleza mageuzi hayo. 

“Kutokana na uzoefu wa wenzetu katika biashara ya sekta ya misitu tayari tumekubaliana na tunakamilisha taratibu za kuanza mradi mwingine mpya ambapo Finland itaisaidia Tanzania Euro milioni 20 kuchagiza mageuzi zaidi kuifanya sekta ya misitu kuisaidia Tanzania,” ameongeza Dkt. Abbasi. 

Dkt. Abbasi ameongoza ujumbe wa wataalamu ambao ni Mkurugenzi wa Idara ya Misitu na Nyuki, Dkt. Deusdedit Bwoyo na Kamishna wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS), Prof. Dos Santos Silayo.


Ufini ndio nchi inayoongoza Barani Ulaya kwa kuwa na eneo lenye misitu mingi, sehemu kubwa (asilimia 60) ikimilikiwa na sekta binafsi na asilimia nyingine inayobaki ikiwa chini ya umma ikisimamiwa na kampuni binafsi ya Serikali ya Forestry LTD. Mapato ya Ufini kwa mwaka 2022 kutoka sekta ya misitu yalifikia Euro Bilioni 20 (Zaidi ya TZS Trilioni 60).

Powered by Blogger.