KIHONGOSI: VIJANA MSIKUBALI KUVURUGA AMANI

 


Na Mwandishi wetu,Timesmajira 

KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi amewataka vijana nchini kukataa kutumiwa na watu wasioitakia mema nchi yetu kuvuruga  amani na utulivu wa Watanzania kwa sababu yoyote ile.

Kihongosi ametoa rai hiyo jana alipokuwa akiongea na mamia ya wana CCM na wakazi wa Wilaya ya Urambo Mkoani Tabora kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Kitega Uchumi Mjini hapa.

Amesema kuwa Tanzania imejengwa katika misingi imara ya amani na utulivu na Chama Cha Mapinduzi (CCM) tangu kianzishwe 1977 kimeendelea kusimamia misingi hii kwa gharama zozote, kikihubiri amani, umoja na mshikamano.

‘Katika hili, nawasihi vijana wenzangu msikubali kutumiwa na hawa vibaraka wasioitakia mema nchi yetu kuvuruga amani, umoja na mshikamano wa Watanzania, kataeni mambo ya hovyo, lindeni nchi yenu’, amesema.

 Kihongozi amepongeza kazi nzuri iliyofanywa na waasisi wa Taifa hili, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Aman Karume, hivyo akawataka wanasiasa kuacha mihemko yenye viasharia vya uvunjifu wa amani.

‘Najua wana Urambo mnapenda maendeleo na mnajivunia mazuri yote yaliyofanywa na yanayoendelea kufanywa na serikali yenu ya Chama Cha Mapinduzi, asiwepo mtu wa kuwavuruga, lindeni amani iliyopo’, amesema .

Amesisitiza kuwa Chama Cha Mapinduzi ni chama cha wananchi wote ndiyo maana kimeendelea kusimamia kwa dhati amani, upendo na mshikamano wa watanzania ili tunu hii ya amani iendelee kudumishwa nchini.

Ametaja baadhi ya mambo makubwa yaliyofanywa na serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika Wilaya hiyo kuwa ni kuboreshwa huduma za afya kwa kujengwa hospitali ya wilaya yenye miundombinu yote na kujengwa shule mpya za kisasa za msingi na sekondari.

Ujenzi wa vituo vya afya katika Kata mbalimbali, zahanati katika vijiji vyote, Mradi mkubwa wa Maji wa Miji 28 unaogharimu shilingi bilioni 143, ujenzi wa Bwawa la maji la Kalemela na kupeleka umeme katika vijiji na vitongoji vyote.

Mbunge wa Jimbo la Urambo Magreth Sitta amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa CCM Taifa kwa kuwajali wana Urambo na kuwaletea mabilioni ya fedha kwa ajili ya kutekelezwa miradi ya maendeleo.







Powered by Blogger.