DIARA AFUNGIWA KUCHEZA MICHEZO MITATU NA FAINI YA MILIONI NNE KWA KUMSHAMBULIA MWAMUZI NA KUOMYESHA ISHARA YA KIDOLE CHA KATI
Golikipa wa klabu ya Yanga, Djigui Diarra amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Tsh. milioni mbili kwa kosa la kumshambulia mwamuzi wa kati wa mchezo wao wa sare ya 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, mara baada ya mchezo huo kumalizika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Sambamba na adhabu hiyo iliyotolewa leo Machi 27, 2026 na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Machi 26, 2026, Diarra pia ametozwa faini ya milioni mbili kwa kosa la kuonesha kidole cha kati wakati akitoka uwanjani baada ya kumalizika kwa mchezo huo.
Aidha Mwamuzi wa kati wa mchezo huo, Gilbert Mrina kutoka Kilimanjaro, ameshushwa Daraja la Uamuzi kwa kosa la kushindwa kuchukua hatua stahili kwa Diarra kwa kitendo hicho cha utovu wa nidhamu (kumshambulia mwamuzi) kama ilivyoainishwa kwenye Kanuni ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.
Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia kuwa ni kosa la kujirudia ambapo mwamuzi Gilbert Mrina alitenda kosa la aina hiyo katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC kati ya Mbeya City dhidi ya Namungo FC na akaadhibiwa kwa kufungiwa mizunguko mitatu.

