RAIS DKT.MWINYI AKUTANA NA UONGOZI WA KITUO CHA ZRCP
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ameushauri uongozi wa Kituo cha Tafiti za Kiuchumi, Kijamii na Uchambuzi wa Sera Zanzibar (ZRCP) kuandaa mikutano na mijadala na wadau ili kuwaelimisha umuhimu wa kutumia matokeo ya tafiti katika utekelezaji wa majukumu yao.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 24 Machi 2026, alipokutana na Mkurugenzi Mkuu wa kituo hicho, Ndugu Juma Reli, pamoja na ujumbe wake waliofika Ikulu, Zanzibar.
Aidha, amebainisha umuhimu wa kufanya maboresho katika mifumo ya usajili wa malipo ya kidijitali ili kuimarisha muda na uwazi, hususan katika sekta ya umma, na kushauri kuangaliwa upya kwa sera, sheria na kanuni katika eneo hilo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Tafiti za Kiuchumi, Kijamii na Uchambuzi wa Sera Zanzibar (ZRCP), Ndg. Juma Hassan Reli, ameunga mkono mapendekezo hayo na kueleza kuwa kituo hicho kipo tayari kushirikiana na Serikali katika kutoa tafiti na mapendekezo yatakayochangia maboresho ya mifumo ya malipo ya kidijitali, ikiwa ni pamoja na kusaidia mapitio ya sera, sheria na kanuni ili kuimarisha uwazi na ufanisi katika sekta ya umma.

