OASIS YAIPONGEZA TRA KWA MABORESHO YA MIFUMO YA KITEKNOLOJIA YA ULIPAJI KODI


Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya OASIS Financial Services Ltd, Bw. Stambuli Myovela, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kufanya maboresho makubwa ya mifumo ya kiteknolojia katika ukusanyaji na ulipaji wa kodi, hatua iliyorahisisha huduma kwa walipakodi ndani na nje ya nchi.


Amesema kuwa TRA imepiga hatua kutoka mifumo ya kizamani na kuingia katika mfumo wa kisasa wa kidigitali, unaowawezesha walipakodi kulipa kodi na kuwasiliana na mamlaka hiyo kutoka sehemu yoyote duniani.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Machi 23, 2026, baada ya mafunzo yaliyoandaliwa na TRA kwa kushirikiana na jumuiya ya wafanyabiashara wa Kichina pamoja na OASIS Financial Services Ltd, Myovela alisema mifumo hiyo imeongeza ufanisi na kuvutia wawekezaji zaidi.


Mafunzo hayo pia yalihudhuriwa na Kamishna wa TRA, Bw. Yusuph Mwenda, pamoja na Balozi wa China nchini Tanzania, ambapo viongozi hao walionesha dhamira ya kushughulikia changamoto za kikodi zinazowakabili wafanyabiashara.


Myovela alifafanua kuwa mifumo ya kidigitali ya TRA imeongeza uwazi na uaminifu katika ukusanyaji wa kodi, kwani imeunganishwa na mifumo mingine ya Serikali, hivyo kufanya makadirio ya kodi kuwa sahihi zaidi kuliko mfumo wa makadirio ya kubahatisha.


“Kuanzia usajili, uwasilishaji wa ritani, upatikanaji wa cheti cha kodi (Tax Clearance Certificate), hadi kushughulikia mapingamizi na mawasiliano ya kikodi, yote yanafanyika kupitia mfumo wa TRA Online,” alisema Myovela.


Aidha, alisisitiza kuwa mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania yanaendelea kuwa mazuri kutokana na uwepo wa rasilimali nyingi, jiografia rafiki, utulivu wa kisiasa pamoja na maboresho ya kimfumo yanayoifanya nchi kuwa kivutio kikubwa cha uwekezaji ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika Mashariki.



Kwa upande wa uwekezaji kutoka China, Myovela alisema kuwa katika mwaka 2023/2024, miradi iliyosajiliwa kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ilikuwa na thamani ya dola za Marekani bilioni 1.7 (zaidi ya Sh trilioni 4).


Alibainisha kuwa kati ya miradi hiyo, wawekezaji wa Kichina walichangia dola bilioni 1.053, sawa na asilimia 60 ya uwekezaji wote, hali inayoonesha mchango mkubwa wa wawekezaji hao katika kukuza uchumi wa Tanzania.


Aliongeza kuwa uwekezaji huo umechangia uzalishaji wa bidhaa mbalimbali nchini ikiwemo vigae, vioo, sabuni za unga, vipuri na hata uunganishaji wa magari mapya, hatua inayowa


wezesha Watanzania kujifunza teknolojia na kuendeleza viwanda vya ndani.


Myovela alihitimisha kwa kusema kuwa uwekezaji huo umeleta mapinduzi ya kiteknolojia kupitia uhamishaji wa ujuzi (technology transfer), matumizi ya mashine za kisasa pamoja na kuongeza ajira na masoko kati ya Tanzania na China.


Powered by Blogger.