RAIS SAMIA AWEKA JIWE LA MSINGI, MRADI WA UJENZI WA MATANKI YA KUPOKEA NA KUSAMBAZA MAFUTA, BANDARI YA DAR ES SALAAM
Na Mwandishi wetu,DAR ES SALAAM
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo ameweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Ujenzi wa Matanki ya Kupokea na Kusambaza Mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam.
Rais Dkt. Samia amesema mradi huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na kuiweka Tanzania katika nafasi ya ushindani kama kitovu cha biashara ya kikanda, na ni hatua muhimu ya kudhibiti changamoto za muda mrefu za kupokea na kuhifadhi mafuta kwa lengo la kuimarisha usalama wa nishati nchini.
Akizungumzia maboresho yanayoendelea kufanywa katika bandari, Rais Dkt. Samia amesema hatua ya ushirikishwaji wa sekta binafsi katika uendeshaji wa bandari nchini imeongeza ufanisi, kupanua uwezo wa kuhudumia shehena na kuongeza mapato ya Serikali.
Ameongeza kuwa, mradi wa matanki ya kupokea mafuta utaimarisha uwezo wa bandari katika kuhudumia shehena za mafuta kwa wakati, kupunguza changamoto za kuchelewa kushusha shehena, na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa nishati ya mafuta kwa wananchi na sekta za uzalishaji.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia ameelekeza kuimarishwa kwa Akiba ya Kimkakati ya Hifadhi ya Mafuta (National Strategic Petroleum Reserves), ili kuongeza uwezo wa nchi kukabiliana na misukosuko ya soko la dunia. Aidha, amesisitiza kuimarishwa kwa mifumo ya kisasa ya ufuatiliaji wa shehena za mafuta kuanzia bandarini hadi hatua za usambazaji, kwa lengo la kuweka uwazi na kulinda mapato ya Taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema Serikali inaendelea kuunganisha huduma za bandari na reli ya kisasa (SGR), ambapo usafirishaji
wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Dodoma utaanza rasmi, sambamba na kuanzishwa kwa bandari kavu katika mikoa ya Morogoro, Dodoma na Shinyanga ili kurahisisha mtiririko wa mizigo na kupunguza msongamano bandarini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa, amesema kukamilika kwa mradi huo kutapunguza muda wa kuhudumia meli za mafuta kutoka wastani wa siku 22 hadi siku 7 kwa meli moja.
Ameeleza kuwa, hatua hiyo itaondoa gharama ya Dola za Marekani 25,000 (sawa na Shilingi Milioni 58) inayolipwa kama tozo kutokana na kuchelewa kushusha shehena, gharama inayoathiri bei ya mafuta kwa mtumiaji, pamoja na kuvutia meli nyingi zaidi nchini, na hivyo kuimarisha mapato ya Taifa.
Halikadhalika, amebainisha kuwa mradi huu ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango kabambe wa Maendeleo ya Bandari unaolenga kuongeza ushindani, ufanisi na mchango wa sekta ya bandari katika uchumi wa Taifa, na unalenga kuimarisha hadhi ya Bandari ya Dar es Salaam kama lango la nishati kwa nchi jirani.






