PROPHET IPM ATOA WITO KWA WANAUME KUJITATHIMINI KIUCHUMI 2026, ATANGAZA KIKAO MAALUM MLIMANI CITY
Na Magrethy Katengu. DAR ES SALAAM
Kiongozi wa kidini, Prophet IPM, amesema kuwa mwaka 2026 ni mwaka wa kila mwanaume kujitathimini na kujiuliza atachukua hatua gani ili kujikwamua kiuchumi licha ya changamoto zilizopo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 3, 2026 jijini Dar es Salaam, Prophet IPM amesema wanaume wamekuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi pamoja na majukumu mazito waliyonayo, huku wengi wao wakikosa sehemu ya kusemea au kueleza changamoto zao.
Amesema hali hiyo imepelekea baadhi yao kufanya maamuzi magumu yanayoathiri familia na jamii kwa ujumla.
“Mwaka huu kutakuwa na kikao kikubwa cha kuwakutanisha wanaume wote kuanzia umri wa miaka 18. Kikao hicho kitafanyika Aprili 2, 2026 katika ukumbi wa Mlimani City. Wote mnakaribishwa, kiingilio ni shilingi 50,000 na tutawaandalia chakula cha mchana,” amesema Prophet IPM.
Amebainisha kuwa licha ya IPM kuwa na ibada maalum ya kukutanisha wanaume, mwaka huu wameamua kuwashirikisha wanaume wa dini zote. Miongoni mwa wageni waalikwa ni bilionea Said Lugumi pamoja na mashekhe na wafanyabiashara wengine wakubwa.
Naye bilionea Said Lugumi amethibitisha kwa njia ya simu kuwa atahudhuria kikao hicho na atakuwa mmoja wa wazungumzaji wakuu hivyo amesema atatumia nafasi hiyo kuwatia hamasa vijana kutumia muda wao vyema ili kujikwamua kiuchumi na kukabiliana na changamoto za maisha.
Aidha Kwa mujibu wa waandaaji, mavazi rasmi kwa siku hiyo yatakuwa suti nyeusi, shati jeupe, tai nyekundu, soksi nyeusi na viatu vyeusi.

