WAZIRI MAKONDA ABAINISHA MADUDU,NDANI YA MASHIRIKISHO AWAPA ONYO KWA VIONGOZI
Na Mwandishi Wetu –Dar es Salaam
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda amesema migogoro inayojitokeza katika mashirikisho na vyama vya michezo nchini inaathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta hiyo na kusababisha vipaji vya vijana kupotea.
Makonda amesema baadhi ya migogoro hiyo inatokana na viongozi kung’ang’ania madaraka, kukosekana kwa mawasiliano mazuri miongoni mwa viongozi, vitendo vya rushwa pamoja na ukosefu wa uwazi katika mapato na matumizi ya fedha.
Ametoa kauli hiyo Machi 13, 2026, wakati akizungumza katika mkutano wa Baraza la Michezo la Taifa na viongozi wa vyama na mashirikisho ya michezo uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, Makonda alionya kuwa serikali haitavumilia viongozi wa michezo wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao, akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kukwaza maendeleo ya michezo.
“Viongozi wote wa vyama na mashirikisho ya michezo ambao hawajatekeleza ahadi walizotoa wakati wa kuomba uongozi nitawafuatilia. Nikibaini kuwa uongozi haujafikia hata asilimia 20 ya malengo, nitawaondoa bila huruma, kwa kuwa nafasi hizo zimepatikana kwa kura za wanachama,” amesema Makonda.
Aidha, amewataka viongozi hao kujitathmini na kuona kwa kiwango gani wametekeleza ahadi walizotoa, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano na wanachama ili kufikia matokeo chanya badala ya kuishia kwenye michakato.
Makonda amesema Rais wa Samia Suluhu Hassan ameipa wizara hiyo jukumu la kusimamia maendeleo ya sekta ya michezo na kuhakikisha matokeo bora yanapatikana.
Pia amesisitiza umuhimu wa mashirikisho na vyama vya michezo kufuata katiba zao ili kuepusha migogoro inayorudisha nyuma maendeleo ya michezo nchini. Ameongeza kuwa uwazi katika mapato na matumizi ya fedha ni muhimu kwa ustawi wa taasisi hizo.
Kwa mujibu wa Makonda, kuna baadhi ya viongozi wanaofungua akaunti za fedha nje ya nchi kwa manufaa binafsi, jambo ambalo ni kinyume na maslahi ya mashirikisho na wanachama wake.
Kadhalika, amesema anafahamu kuwa kuna viongozi wanaobadilisha katiba za mashirikisho ili kulinda nafasi zao za uongozi, akisisitiza kuwa katiba hizo zinapaswa kulinda maslahi ya wanachama na maendeleo ya michezo.
Akizungumzia maandalizi ya mashindano ya Africa Cup of Nations, Makonda amewataka vijana kupewa fursa zaidi za kushiriki mashindano mbalimbali ili kuonyesha vipaji vyao.
Amesema Tanzania Football Federation imepewa kipaumbele katika maandalizi ya mashindano hayo.
Vilevile, Waziri Makonda ameagiza Tanzania Basketball Federation kuhakikisha ofisi ya Rais wa shirikisho hilo inakabidhiwa kwa Hasheem Thabeet ndani ya siku mbili kabla ya Jumatatu ijayo, akionya kuwa hatua zaidi zitachukuliwa iwapo agizo hilo halitatekelezwa.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa, Neema Msitha, amesema mkutano huo umetoa fursa kwa wadau wa michezo kujadiliana na kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya sekta hiyo.
Amesema pia sekta ya michezo nchini imepiga hatua kubwa kutokana na juhudi na uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.


