HESLB NA POSTA TANZANIA KUIMARISHA HUDUMA ZA MIKOPO KWA VIJANA
Taasisi ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeingia makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Posta Tanzania, hatua inayolenga kurahisisha huduma za maombi ya mikopo kwa vijana nchini.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo iliyofanyika Aprili 23, 2026, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia, amesema ushirikiano huo utasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wanafunzi wakati wa kuomba mikopo.
Ameeleza kuwa kupitia ofisi za Posta zilizopo maeneo mbalimbali nchini, vijana watapata huduma za kujaza na kuwasilisha maombi ya mikopo, kufanyiwa uhakiki wa nyaraka pamoja na kupatiwa msaada wa kitaalamu ili kuhakikisha wanakidhi vigezo vinavyotakiwa.
“Lengo letu ni kuhakikisha hakuna kijana anayekosa mkopo kwa sababu ya changamoto za kiufundi au kukosa msaada wa kujaza maombi,” alisisitiza Dk. Kiwia.
Ameongeza kuwa tangu kuanzishwa kwa HESLB, zaidi ya shilingi trilioni tisa zimetolewa kama mikopo kwa wanufaika zaidi ya milioni moja, wakiwemo wanafunzi wa shahada, stashahada, uzamili na uzamivu.
Hata hivyo, amekiri kuwepo kwa changamoto katika mifumo ya maombi, hususan kwa vijana walioko maeneo ya vijijini na wale wasio na urahisi wa kupata huduma za mtandao, hali ambayo ushirikiano huo unalenga kuipunguza.
Kwa upande wake, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo, amesema taasisi hiyo itaendelea kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi kupitia mtandao wake wa zaidi ya ofisi 350 nchini pamoja na muunganiko wa kimataifa.
Amebainisha kuwa Posta tayari inashirikiana na taasisi zaidi ya 150 za serikali na binafsi kusambaza huduma mbalimbali ikiwemo vifaa tiba, taarifa na huduma za kifedha.
Amesema kupitia makubaliano hayo mapya, Posta itahakikisha vijana wanapata mwongozo sahihi wa kujaza fomu za mikopo na kuepuka makosa yanayoweza kuwanyima fursa hiyo muhimu.
Hafla hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya juhudi za serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, zinazolenga kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya vijana nchini.



