RAIS DKT. MWINYI AWASISITIZA MABALOZI KUKUZA DIPLOMASIA YA UCHUMI KIMATAIFA

 



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewasisitiza mabalozi wanaoenda kuiwakilisha Tanzania katika mataifa mbalimbali kuweka kipaumbele katika kuzingatia diplomasia ya kiuchumi kwa kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini.



Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 08 Aprili 2026, alipokutana na mabalozi hao waliofika Ikulu, Zanzibar, kumuaga kabla ya kwenda katika vituo vyao vya kazi.



Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewahimiza mabalozi hao kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maslahi ya pande zote mbili za Muungano, pamoja na kuweka kipaumbele katika utekelezaji wa sera kuu ya diplomasia ya uchumi.


Halikadhalika, Rais Dkt. Mwinyi amebainisha kuwa Zanzibar iko tayari kupokea wawekezaji, hususan katika uwekezaji wa miundombinu ikiwemo bandari, viwanja vya ndege, barabara, uvuvi na utalii.




Eneo jengine ambalo Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza ni upatikanaji wa wafanyabiashara na wawekezaji katika zao la mwani, pamoja na wale watakaowekeza katika ununuzi na uongezaji thamani wa zao la karafuu.


Naye Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Balozi Swahiba Mndeme, akizungumza kwa niaba ya mabalozi hao, amemuhakikishia Rais Dkt. Mwinyi kuwa wameyapokea na watayatekeleza maelekezo yake kwa vitendo na kuitangaza kikamilifu diplomasia ya uchumi.


Mabalozi walioaga ni Balozi Mhandisi Zena Ahmed Said (Saudi Arabia), Balozi Cyprian John Luhemeja (Zambia), Balozi Maulidah Bwanaheri Hassan (Oman), Balozi Salim Othman Hamad (Comoros), Balozi Swahiba Habib Mndeme (Sweden), Balozi Noel Emmanuel Kaganda (Korea) na Balozi Mussa Haji Ali, Naibu Mwakilishi wa Kudumu Umoja wa Mataifa, New York.




Powered by Blogger.