AKAMATWA NA POLISI KWA UTOAJI WA MIMBA
Na Mwandishi wetu, TABORA
JESHI la Polisi Mkoani Tabora linamshikilia mwanamke mmoja (21) mkazi wa Mtaa wa Singo, Kata ya Gongoni katika halmashauri ya manispaa Tabora kwa tuhuma za kutoa ujauzito wake unaokadiriwa kuwa na umri wa miezi 6.
Kamanda wa Polisi Mkoani hapa Richard Abwao amethibitisha kutokea tukio hilo Aprili 6 mwaka huu majira ya saa 12.45 za jioni katika Kata hiyo ambapo mwanamke huyo mpare, mkristo na mkulima aligundulika kufanya kitendo hicho.
Amesema kuwa mtuhumiwa baada ya kumeza dawa ya kutoa ujauzito huo, uchafu aliuweka kwenye kopo na kuufunga kwenye mfuko ili akautupe kwenye shimo la takataka lililo jirani na eneo hilo.
Kamanda ameongeza kuwa mbali na mtuhumiwa huyo pia wamemkamata mwanaume mmoja (25) msukuma, mkazi wa Kata ya Chemchem katika manispaa hiyo ambaye ni Mtaalaumu wa Maabara aliyempatia dawa za kutolea mimba hiyo.
Ameeleza sababu ya kutoa ujauzito huo kuwa ni mwanaume aliyempa mimba hiyo kuikataa hivyo akaamua kwenda kwa Mtaalaumu binafsi wa Maabara ili ampatie dawa za kuitoa.
Kamanda Abwao amedokeza kuwa mwanamke huyo amepewa fomu namba 3 na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo, Kitete, kwa ajili ya matibabu na uchunguzi zaidi wa afya yake chini ya uangalizi wa Polisi.
‘Kutoa ujauzito ni kosa la kisheria, kwa sababu unakatisha uhai wa kiumbe kilichoko tumboni, hata madhehebu ya dini zetu yanakataza kutoa mimba, hili ni kosa’, ameeleza.
Uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili watuhumiwa hao bado unaendelea na watafikishwa mahakamani mara tu utakapokamilika.
Kamanda ametoa wito kwa jamii kuacha kuchukua maamuzi hatarishi kwa afya zao wanapokuwa na migogoro ya kifamilia bali watumie njia sahihi kuwasilisha malalamiko yao ili yatatuliwe kwa wakati na sio kujichukulia sheria mkononi.

