RUWASA KIGOMA WAMWAGA PONGEZI KWA RAIS SAMIA

 


WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoani Kigoma wameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia zaidi ya shilingi bilioni 79 za miradi ya maji.

Pongezi hizo zimetolewa jana na Meneja wa Wakala huo Mkoani hapa Mhandisi Mathius Mwenda alipokuwa akiongea kwenye mahojiano maalumu na waandishi wa habari Ofisini kwake.

Amesema kuwa RUWASA Kigoma ina kila sababu ya kuishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kufanikisha utekelezaji miradi mbalimbali ya maji katika Wilaya zote 7 za Mkoa huo hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa kero ya maji.

Mhandisi Mwenda amebainisha kuwa kuanzia Machi 2021 hadi Februari 2026, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alitenga zaidi ya shilingi bilioni 79 kwa ajili ya kutekeleza miradi 113 ya maji katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo.

Amedokeza kuwa kati ya kiasi hicho cha fedha, serikali ilitoa jumla ya shilingi bilioni 55.9 na wadau wakaiunga mkono kwa kutoa kiasi cha shilingi bilioni 23.4  ili kufanikisha utekelezaji miradi hiyo.

‘Hadi kufikia mwezi Februari mwaka jana jumla ya miradi 93 kati ya 113 iliyoanza kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita imekamilika kwa asilimia 100, na wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama ya bomba’, amesema.

Ameongoza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kumewezesha wakazi zaidi ya laki 8 wa Mkoa huo kuanza kupata maji safi ya bomba katika maeneo yao huku miradi 20 iliyobakia ikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.  

Mwenda amefafanua kuwa utekelezaji miradi hiyo ulilenga kujenga miradi mipya, kufanya upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya maji, utafutaji wa vyanzo vya maji, maandalizi ya miradi mipya na uchimbaji wa visima virefu.

Ameongeza kuwa Wizara ya Maji imeingia Mkataba na Mhandisi Mshauri, Kampuni ya ICE Project ya Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kusanifu Mradi Mkubwa wa maji kutoka chanzo cha Ziwa Tanganyika utakaoongeza usambazaji  maji katika Mikoa 3 ya Kigoma, Katavi na Rukwa.

Amedokeza kuwa timu ya Wahandisi Washauri ilifika Mkoani humo  mwezi Machi, mwaka huu kwa ajili ya kujitambulisha na kuanza kazi rasmi ya usanifu, kukamilika kwa mradi huo kutaondoa kabisa kero ya maji katika Mkoa huo.





Powered by Blogger.