(UMALITA) WAMSHUKURU RAIS DKT SAMIA KWA KUHUDHURIA KONGAMANO LAO DAR ES SALAAM
Chama cha Mama Lishe na Baba Lishe Tanzania (UMALITA) kimemshukuru Samia Suluhu Hassan kwa kuhudhuria na kuwa mgeni rasmi katika kongamano lao lililofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Shukrani hizo zimetolewa Aprili 21, 2026 na Mwenyekiti wa UMALITA, Vijawa Omari, mara baada ya kuhitimishwa kwa kongamano hilo. Amesema hapo awali kundi la Mama Lishe na Baba Lishe lilikuwa halitambuliwi ipasavyo, hali iliyosababisha kukosa fursa mbalimbali ikiwemo mikopo na maeneo rasmi ya kufanyia biashara.
Ameeleza kuwa ujio wa Rais katika kongamano hilo umeleta matumaini mapya, hasa baada ya kutoa maelekezo mbalimbali kwa taasisi husika ili kuhakikisha wanapatiwa huduma stahiki na kutatuliwa changamoto zao.
“Kwa hakika tumefarijika sana kumuona Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akihudhuria kongamano letu kama mgeni rasmi. Hii ni ishara kwamba sasa tunatambulika na kuthaminiwa. Maelekezo aliyoyatoa yakitekelezwa yatatuinua kiuchumi kutoka hatua moja kwenda nyingine,” amesema Vijawa.
Aidha, amesema UMALITA inapanga kufanya ziara nchi nzima kwa lengo la kukutana na Mama Lishe na Baba Lishe, kuwahamasisha kujiunga na chama hicho pamoja na kuwaelimisha kuhusu fursa zilizopo, ikiwemo upatikanaji wa mikopo na umuhimu wa kujisajili ili kutambulika rasmi wanapohitaji huduma za serikali.




