UMEME WAWASHA TUMAINI JIPYA MWAMBAO WA ZIWA NYASA

 


Na Mwandishi Wetu, Ludewa – Njombe

Matumaini ya ukuaji wa uchumi na uboreshaji wa huduma za kijamii yameongezeka kwa wakazi wa mwambao wa Ziwa Nyasa, wilayani Ludewa mkoani Njombe, kufuatia juhudi za Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kusogeza huduma ya umeme katika vitongoji mbalimbali vya eneo hilo.

Hatua hiyo imekuja sambamba na ziara ya Bodi ya Nishati Vijijini (REB) iliyolenga kukagua maendeleo ya miradi ya umeme, ambapo imeelezwa kuwa kiasi cha shilingi bilioni 3.2 kimetengwa kwa ajili ya kukamilisha usambazaji wa nishati hiyo katika wilaya ya Ludewa.

Akizungumza katika ziara hiyo iliyofanyika katika Shule ya Msingi Lumbila, Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, John Mwasoso, alisema ujio wa umeme ni mkombozi mkubwa katika sekta ya elimu, kwani utaboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji. Alibainisha kuwa tayari maandalizi ya awali yameanza, ikiwemo uwekaji wa mifumo ya nyaya (wiring) kwenye madarasa na nyumba za walimu.

Kwa upande wao, wananchi wa Kitongoji cha Mabatini wameeleza matumaini makubwa ya kunufaika kiuchumi kupitia nishati hiyo, hususan katika sekta ya uvuvi. Mkazi wa eneo hilo, Augustino Madesu, alisema upatikanaji wa umeme utawawezesha kuhifadhi samaki kwa kutumia majokofu, hivyo kuepuka hasara ya kuuza samaki kwa bei ya chini wakati wa mavuno mengi.

Naye Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Nkanda, Timotheo Nkwabi, alieleza kuwa huduma za afya zitaboreshwa kwa kiasi kikubwa, hasa katika utoaji wa huduma wakati wa usiku pamoja na matumizi ya mifumo ya kidigitali katika utunzaji wa kumbukumbu za wagonjwa na dawa.

Akizungumza kwa niaba ya Bodi ya Nishati Vijijini, Mkurugenzi wake, Mhandisi Ahmed Chinemba, aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali imeweka kipaumbele kwa taasisi za umma kama shule, zahanati na miradi ya maji ili kuhakikisha manufaa ya umeme yanafika kwa haraka kwa wananchi.

“Tunawahamasisha wananchi kujiandaa kwa kufanya ‘wiring’ kwenye majengo yao ili waweze kuupokea umeme mara tu unapofika. Lengo letu ni kuona nishati hii inabadilisha maisha ya Mtanzania wa vijijini,” alisema Chinemba.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja Msimamizi wa Miradi REA, Mhandisi Deogratius Nagu, alisema kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma hiyo, Bodi imeelekeza kuongeza idadi ya wanufaika ili kaya nyingi zaidi ziweze kupata umeme kabla ya kukamilika kwa mradi huo.

Kukamilika kwa mradi huo kunatarajiwa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa kufungua fursa za ajira kwa vijana kupitia uanzishaji wa viwanda vidogo, saluni na biashara nyingine zinazotegemea nishati ya umeme, huku pia ukichochea maendeleo ya kijamii na kuimarisha usalama katika mwambao wa Ziwa Nyasa.

Powered by Blogger.