USALAMA DAR WAZIDI KUIMARIKA, WATUHUMIWA 37 WAKAMATWA KWA UHALIFU MTANDAONI

 


Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Jumanne Murilo, amesema hali ya kiusalama katika Jiji la Dar es Salaam kwa sasa ni shwari kufuatia juhudi kubwa zinazofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi katika kudhibiti uhalifu.


Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Aprili 27, 2026, Murilo amesema hali hiyo ni tofauti na siku za nyuma, ambapo kumekuwa na mafanikio makubwa katika kuimarisha ulinzi na usalama kupitia ushirikiano madhubuti kati ya vyombo vya dola na wananchi.


Ameeleza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuzuia na kudhibiti vitendo vya kihalifu kwa kutumia taarifa zinazotolewa na wananchi pamoja na wadau wengine wa usalama, hatua inayochangia kwa kiasi kikubwa kupunguza uhalifu katika jiji hilo.


Katika operesheni maalum iliyofanyika Aprili 20, 2026 eneo la Ubungo, Polisi waliwakamata watu 37 kwa tuhuma za kujihusisha na makosa ya kimtandao, ikiwemo kutoa vitisho na kutumia lugha chafu kwa njia za kidijitali, huku baadhi yao wakidaiwa kuwa wafanyakazi wa kampuni za ukopeshaji fedha mtandaoni.


Murilo ametaja baadhi ya watuhumiwa hao kuwa ni Renatus Mujwahuzi maarufu ‘Migeyo’, Odilia Oswin ‘Ngunga’, Theresia Brastius ‘Kanu’ pamoja na wenzao 34, akibainisha kuwa hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa ili kuwafikisha kwenye vyombo husika vya sheria.


Aidha, ameeleza kuwa katika kipindi cha Machi hadi Aprili 2026, mahakama mbalimbali jijini Dar es Salaam zimetoa hukumu kali kwa wahalifu, ikiwemo vifungo vya maisha na miaka 30 jela kwa makosa ya ubakaji, ulawiti na unyang’anyi wa kutumia silaha, hatua inayoonesha dhamira ya dhati ya serikali katika kupambana na uhalifu.


Amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao, huku akitoa wito kwa jamii kuendelea kutoa taarifa za viashiria vya uhalifu na kujitokeza mahakamani kutoa ushahidi ili kuhakikisha haki inatendeka na usalama unaendelea kuimarika.

Powered by Blogger.