ACT WAZALENDO YATANGAZA BARAZA KIVULI JIPYA, YAAHIDI KUIBANA SERIKALI NA KUSISITIZA UWAJIBIKAJI

 




Chama cha ACT Wazalendo kimetangaza rasmi Baraza Kivuli jipya la Mawaziri kwa kipindi kinachofuata baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, kikiahidi kuendelea kuisimamia Serikali kwa nguvu zaidi ndani na nje ya Bunge.


Akizungumza leo Mei 18, 2026, Kiongozi wa chama, Dorothy Jonas Semu, alisema matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 yameendelea kutoa uwakilishi mwembamba wa upinzani Bungeni, hali inayovifanya vyama vya siasa kutumia mifumo mbadala ya kuisimamia Serikali na kuhakikisha uwajibikaji kwa wananchi unaendelea kuwepo.


Semu alisema ACT Wazalendo itaendelea kusimamia siasa za hoja kupitia Baraza Kivuli lililoanzishwa rasmi kwa Azimio la Halmashauri Kuu ya Taifa mwaka 2022. Alisema azimio hilo lilimpa mamlaka Kiongozi wa Chama kuunda Baraza hilo ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kupata sauti mbadala yenye nguvu hata nje ya mhimili wa Bunge.


Kwa mujibu wa Semu, hili ni Baraza la tatu tangu kuanzishwa kwake mwaka 2022, ambapo kwa miaka minne iliyopita limekuwa jukwaa muhimu la kuibua changamoto za wananchi, kushawishi mjadala wa kitaifa kuhusu masuala ya msingi na kuisukuma Serikali kuchukua hatua mbalimbali za kisera na kiutendaji.


Alisema Baraza jipya litakuwa tofauti kidogo na yaliyopita kwa kuwa litawahusisha pia wabunge waliopo Bungeni sambamba na wataalamu na wanachama wenye uzoefu waliopo nje ya Bunge, hatua inayolenga kupanua wigo wa usimamizi wa Serikali na kuongeza ubora wa utendaji wake.


Katika uteuzi huo, Semu alisema uwiano wa kijinsia umezingatiwa ambapo wanawake 11 kati ya wasemaji 23 wameteuliwa, sawa na asilimia 47 ya wajumbe wote wa Baraza hilo.


Katika nafasi za juu za uongozi wa Baraza Kivuli, Isihaka Rashid Mchinjita ameteuliwa kuwa Waziri Mkuu Kivuli huku Luhaga Joelson Mpina akiteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu Kivuli pamoja na Waziri wa Nishati na Madini. Nafasi ya Katibu Mkuu Kiongozi imechukuliwa na Idrisa Abdul Kweweta.


Wengine walioteuliwa ni pamoja na Nagy Kaboyoka ambaye atakuwa Msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu pamoja na Mnadhimu wa Baraza, Ado Shaibu Ado katika Ofisi ya Rais Mipango, Fedha na Hifadhi ya Jamii, na Pavu Abdallah Juma katika Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora.


Majina mengine ni pamoja na Kulthum Jumanne Mchuchuli, Said Ali Mbarouk, Rashid Habib Ali, Peter Madeleka, Fatma A. Fereji, Dkt. Elizabeth Sanga na Riziki Shahari Ngwali miongoni mwa wasemaji wa kisekta walioteuliwa.


Akieleza mwelekeo wa Baraza hilo kwa mwaka huu, Semu alisema wajumbe wote wanapaswa kuweka nguvu kubwa katika kusimamia uwajibikaji serikalini na ndani ya taasisi zake.


Alisema taifa haliwezi kuendelea kujengwa katika misingi ya matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu wa rasilimali za umma na kutowajibika kwa viongozi bila kuwepo sauti thabiti ya kuhoji na kusimamia maslahi ya wananchi.


Katika hotuba yake, Semu aliishutumu Serikali kwa kile alichodai ni matumizi mabaya ya rasilimali za taifa na ukosefu wa uwajibikaji, akisema kupitia uchambuzi wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), chama hicho kimebaini zaidi ya shilingi trilioni saba zimepotea au kutumika bila maelezo ya kuridhisha.


Aidha, alieleza kuwa taifa limeendelea kushuhudia matukio ya mauaji, uporaji wa ardhi za wananchi na matumizi yasiyoeleweka ya fedha za umma huku kukiwa hakuna hatua madhubuti za uwajibikaji zinazochukuliwa.


Kutokana na hali hiyo, Semu aliwataka wajumbe wote wa Baraza Kivuli kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kupigania uwajibikaji wa viongozi, matumizi sahihi ya fedha za umma, ulinzi wa haki za wananchi na utawala unaozingatia sheria na haki.


“ACT Wazalendo itaendelea kuwa sauti ya wananchi waliokata tamaa ya kusikilizwa, na Baraza hili litakuwa mstari wa mbele kuhakikisha hakuna anayekuwa juu ya sheria wala anayefanya matumizi mabaya ya mamlaka bila kuhojiwa,” alisema Semu.

Powered by Blogger.