IZO BATTERY YAZINDULIWA DAR, HAITUMII MAJI YATIKISA SOKO KWA UBORA NA WARANTI YA MIAKA MITANO

 



Kampuni ya Izo Motor’s Company LTD leo Mei 12, 2026 imezindua rasmi bidhaa mpya ya betri za magari zinazojulikana kama “Izo Battery”, zikiwa na teknolojia ya kipekee  ya kutotumia maji katika matumizi yake pamoja na kudumu kwa muda mrefu.


Uzinduzi huo umefanyika jijini Dar es Salaam ambapo kampuni hiyo yenye makao yake Kariakoo katika eneo la Narung’ombe na Limumba, imeeleza kuwa ujio wa betri hizo ni sehemu ya kutoa suluhisho la upatikanaji wa betri bora za magari kwa bei nafuu kwa Watanzania.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, balozi wa bidhaa hiyo ambaye pia ni mshawishi maarufu mitandaoni, Dotto Magari amesema kuwa betri hizo hazitumii maji bali zinatumia mfumo wa “dry battery”, jambo linalorahisisha matumizi kwa wateja huku kampuni ikitoa waranti ya miaka mitano kwa kila betri.


Amesema mazingira mazuri ya uwekezaji nchini yameiwezesha kampuni hiyo ya wazawa kuwekeza katika uzalishaji wa betri hizo, hatua ambayo pia imechangia kuongeza ajira kwa Watanzania pamoja na kukuza uchumi wa taifa.


“Tunazo aina mbalimbali za betri katika saizi tofauti zinazokidhi mahitaji ya magari mbalimbali. Bidhaa hizi zinapatikana kwa bei nafuu kwa jumla na rejareja, zimepunguzia madereva na Wamiliki wa Magari kutotembea vidumu vya Maji ” amesema Dotto Magari.


Aidha amesema ushirikiano wake na kampuni hiyo utaisaidia “Izo Battery” kuwafikia Watanzania wengi zaidi pamoja na kupanua soko la bidhaa hizo kimataifa.


“Kampuni ya Izo Battery imeingia makubaliano na mimi kuwa balozi wake. Ninaamini kupitia ushirikiano huu bidhaa hizi zitaendelea kujenga imani kubwa kwa watumiaji kutokana na ubora wake,” ameongeza.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Izo Motor’s Company Ltd, Bw. Izo Mahenge amesema betri hizo zimetengenezwa kwa viwango vya ubora wa hali ya juu ili kuhimili ushindani wa soko huku vikiwa na nembo ya Made in Tanzania kuhakikishia Wazawa kuwa imezalishwa hapa Nchini kwao


“Izo Battery zinazalishwa hapa Tanzania. Ni betri bora na imara, watumiaji wa magari wazitumie Izo Battery hawatajuta kwani inawaondolea kero ya kitembeà na madumu ya Maji ,” amesema Mahenge.


Ameongeza kuwa kampuni hiyo imeendelea kutoa ajira kwa Watanzania ambapo zaidi ya watu 60 wameajiriwa katika kiwanda hicho huku kampuni ikiwa na mawakala zaidi ya 70 wanaosambaza bidhaa hizo nchi nzima.


“Tumekuja na kitu tofauti sokoni, lengo letu ni kuhakikisha Watanzania wanapata bidhaa bora zinazotengenezwa hapa nchini,” amesema.

Powered by Blogger.