KAWAANDAENI VIJANA WA KITANZANIA KUWA WABUNIFU, WAJASIRIAMALI, WASHINDANI KATIKA AJIRA - PROF. SHEMDOE

 


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amewataka walimu wapatao 150 wa shule za amali waliopatiwa mafunzo nchini India kwenda kuwapatia ujuzi vijana wa kitanzania katika shule wanazofundisha ambao utawawezesha kuwa wabunifu, wajasiriamali na washindani katika ajira za ndani na nje ya nchi ili kutoa mchango katika maendeleo ya taifa.

 

Prof. Shemdoe ametoa wito huo Mei 04, 2026 wakati wa kikao chake na walimu hao wapatao 150 wa Shule za Amali ambao wamerejea nchini kutoka nchini India walihudhuria mafunzo ya kuwajengea



uwezo wa kutoa elimu ya ufundi na mafunzo ya stadi za kazi kama nyenzo muhimu ya kukuza uchumi wa viwanda, kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana, na kuongeza ushindani katika soko la ajira.


“Tunategemea vijana watakaotoka katika shule za amali wawe na uwezo wa kushindana katika ajira za ndani na nje ya nchi, waweze kujiajiri na kuwa wajasiriamali wenye mchango kwa taifa, hivyo muwapatie ujuzi na maarifa yote mliyoyapata nchini india,” amesisitiza Prof. Shemdoe.


Aidha, Prof. Shemdoe amewataka walimu hao kwenda kuwafundisha walimu ambao hawakupata fursa kupata mafunzo nchini India na kuongeza kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu watawasilisha ombi kwa Mhe. Rais la kupatiwa fedha za kwenda kuwajengea uwezo walimu wa amali 601 waliosalia ili wawe na tija katika Taifa.


Prof. Shemdoe amempongeza Waziri wa Elimu na timu yake pamoja na Katibu Mkuu-TAMISEMI na timu yake kwa kushirikiana na Washauri Elekezi Global Education Link kuratibu zoezi la walimu hao wapatao 150 wa amali kwenda nchini India kupatiwa mafunzo yatakayowezesha utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu.


Mmoja wa walimu walionufaika na mafunzo hayo, Mwalimu Paul Maziku wa Shule ya Sekondari Chato amesema wamefundishwa namna ya kuwawezesha wanafunzi kufikia ndoto zao na malengo yaliyokusudiwa na Serikali ya kuwa na elimu ya amali na kuongeza kuwa, walimu wote wapatao 150 waliopatiwa mafunzo wana ari ya kufundisha ili kuleta mabadiliko katika elimu.


Naye mnufaika mwingine wa mafunzo, Mwalimu Sungura Mollel wa Shule ya Sekondari ya Amali Ruvuma amesema kuwa wakiwa nchini India, wamejifunza namna ya kuandaa mitaala kulingana na uhitaji wa viwanda hivyo anaamini kwamba ujuzi walioupata utawawezesha kuwaandaa vijana wa kitanzania kuwa na ujuzi wenye tija kwa taifa ikizingatiwa kwamba wao ni walezi.

Powered by Blogger.