WANANCHI DODOMA WAPONDEZA JUHUDI ZA SERIKALI KATIKA KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

 

Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Wananchi wa Jiji la Dodoma wamepongeza juhudi za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, wakisema mkakati huo unachangia kuboresha afya za wananchi, kuokoa muda na kulinda mazingira.


Pongezi hizo zimetolewa leo Mei 4, 2026 katika Soko la Mavunde, eneo la Chang’ombe, ambapo wananchi walipata elimu ya nishati safi ya kupikia kupitia mafunzo ya nadharia na vitendo.


 Mafunzo hayo yalilenga kuwawezesha wananchi kuelewa matumizi sahihi na yenye ufanisi ya nishati hizo katika shughuli za kila siku za upishi.


Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema elimu ya vitendo waliyoipata imewasaidia kufahamu kwa urahisi faida za nishati safi, ikiwemo kupunguza moshi majumbani unaosababisha magonjwa ya njia ya hewa pamoja na kurahisisha shughuli za upishi.


Mkazi wa Kata ya Chang’ombe, Aisha Ramadhani, amesema kampeni hiyo imebadilisha mtazamo wake kuhusu matumizi ya nishati, akieleza kuwa sasa anatambua umuhimu wa kuachana na kuni na mkaa na badala yake kutumia nishati safi kwa ajili ya afya bora na uhifadhi wa mazingira.


Kwa upande wake, mtaalamu kutoka Wizara ya Nishati, Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, Nsajigwa Maclean, amesema Serikali inaendelea kuhakikisha nishati safi inapatikana kwa urahisi na kwa gharama nafuu ili kuwafikia wananchi wote bila kujali kipato au eneo wanaloishi.


Ameongeza kuwa Serikali imejikita pia katika kutoa elimu endelevu kwa jamii kupitia mafunzo ya vitendo, hatua inayolenga kuongeza uelewa wa matumizi salama ya nishati safi na kuhamasisha mabadiliko ya tabia kutoka matumizi ya kuni na mkaa kwenda kwenye nishati mbadala rafiki kwa afya na mazingira.


Wananchi walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kuridhishwa na juhudi hizo na kuahidi kuwa mabalozi wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika jamii zao.

Powered by Blogger.