MAFUNDI WAKEMEA SIASA ZA VURUGU.

 


- Wasema Tanzania haiwezi kuendeshwa kwa taharuki, wananchi wa kawaida ndio hubeba gharama za machafuko


Baadhi ya Mafundi ujenzi, kuchomea na kushona viatu jijini Dar es salaam wameungana kukemea matumizi ya vurugu, maandamano na uchochezi wa kisiasa kama mbinu ya kutafuta mafanikio ya kisiasa, wakisisitiza kuwa Tanzania haiwezi kuendeshwa kwa siasa za taharuki, hasira na uvunjifu wa amani.


Kauli hizo zimetolewa leo walipo hojiwa na mwandishi wa habari hii kujua mapokeo ya wananchi kutokana na kusambaa kwa barua waliyoandikiwa chama cha Demokrasia na Maendeleo kikitakiwa kujieleza kwanini kisichukuliwe hatua kutokana na uvunjifu wa sheria ya vyama vya siasa


*“UCHOCHEZI SIO DEMOKRASIA.”*


Wakizungumza kwa nyakati tofauti, mafundi hao walieleza kuwa baadhi ya wanasiasa wameanza kutumia lugha na mbinu zinazoweza kuhamasisha taharuki, vurugu na migogoro huku wakitaka jamii ionekane kuwa hatua za kisheria dhidi yao ni vita dhidi ya demokrasia.


Abdallah Juma ambaye ni fundi ujenzi alisema Tanzania imejengwa kwenye misingi ya amani, mshikamano na kuheshimu sheria hivyo hakuna nafasi ya siasa za vurugu nchini.


“Tanzania sio nchi ya vurugu, hizi mbinu wanazotaka kutumia hazitasaidia chochote zaidi ya kuwaumiza wananchi wa kawaida,” alisema Abdallah Juma.


Kwa upande wake, fundi mwingine wa ujenzi Musa Mrisho aliwataka wananchi kupuuza wanasiasa wanaohamasisha vurugu, maandamano yasiyo na utulivu pamoja na kauli zinazoweza kuhatarisha amani ya taifa.


Alisema wananchi wa kawaida ndio wanaobeba gharama kubwa za machafuko ya kisiasa kupitia:

kuporomoka kwa biashara,

hofu ya maisha,

kuyumba kwa shughuli za uzalishaji,

pamoja na kukosekana kwa utulivu katika maeneo yao ya kazi na biashara.


“Wanasiasa wakiondoka wananchi ndio wanaobaki na majeraha ya vurugu. Ndiyo maana Watanzania wanapaswa kulinda amani yao,” alisema Musa Mrisho.


Naye Ally Said Nyange ambaye ni fundi uchomeleaji alisema matukio ya vurugu yaliyotokea Oktoba 29 yaliwaathiri zaidi wananchi wa kawaida huku viongozi wa kisiasa wakiendelea na shughuli zao kama kawaida.


“Hakuna mtoto wa mwanasiasa mkubwa aliyeumia, wanaoathirika siku zote ni wananchi wa kawaida,” alisema Ally Said Nyange.


Aliongeza kuwa baadhi ya watu wanaotaka kuhamasisha vurugu wanapaswa kutambua kuwa Tanzania imejengwa kwenye msingi wa umoja na amani hivyo wananchi hawawezi kuunga mkono siasa zinazoweza kuligawa taifa au kuingiza hofu kwa wananchi.


Kwa upande wa mafundi viatu, Landoria Athuman Kajonje alisema baadhi ya viongozi wa CHADEMA wanapaswa kuheshimu utawala wa sheria badala ya kushinikiza Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, aachiwe bila kufuata taratibu za kisheria.

“Kuna Watanzania wengi wamekamatwa sehemu mbalimbali lakini hawana watu wa kuwaandalia kampeni za kuwaachiwa. 


Sheria lazima ifanye kazi kwa kila mtu bila upendeleo,” alisema Landoria Athuman Kajonje.


Naye Zurukifa Juma Luvanga alisema wananchi wa kawaida ndio hubeba gharama kubwa za machafuko ya kisiasa kupitia kuporomoka kwa biashara, hofu ya maisha pamoja na kuyumba kwa shughuli za uzalishaji.

Alisema hali yoyote ya taharuki inapojitokeza, waathirika wakubwa huwa ni wananchi wanaotegemea shughuli za kila siku kujikimu huku viongozi wa kisiasa wakiendelea na maisha yao kawaida.


“Amani ikivunjika wanaoumia ni sisi wananchi wa kawaida ndiyo maana tunasema siasa zifanyike kwa hoja na sheria, si kwa vurugu,” alisema Zurukifa Juma Luvanga.


Aidha, mafundi hao waliipongeza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa kuiandikia CHADEMA barua ya kuitaka ijieleze kwanini isichukuliwe hatua za kisheria kutokana na mwenendo wa baadhi ya viongozi wake.


Kwa mujibu wao, hatua hiyo inaonyesha kuwa hakuna aliye juu ya sheria,

taasisi za nchi zina wajibu wa kulinda amani,

na demokrasia haiwezi kutumiwa kama kinga ya uchochezi au uvunjifu wa sheria.


Walisisitiza kuwa jamii inapaswa kuelewa kuwa suala linaloendelea si vita dhidi ya upinzani bali ni wajibu wa taasisi kuhakikisha sheria zinafuatwa na amani ya nchi inalindwa.


Kwa pamoja mafundi hao walihitimisha kwa kusisitiza kuwa “DEMOKRASIA SIO UCHOCHEZI.”

Na kuongeza kuwa

“Siasa zifanyike kwa hoja na sheria, si kwa taharuki, vurugu na kuhamasisha wananchi kuvunja amani ya nchi yao.”

Powered by Blogger.