MCB BENK YAZINDUA MPANGO WA UUZAJI WA HISA STAHIKI.

 




Uuzaji wa hisa za Benki ya Biashara ya Mwalimu (MCB) ni chachu ya kuimarisha mtaji na kupanua wigo wa utoaji wa mikopo nafuu kwa walimu, wafanyakazi pamoja na wafanyabiashara nchini.


Hayo yamesemwa leo Mei 6,2026 na Waziri Mkuu Mstaafu Kassim Majaliwa wakati wa uzinduzi wa mpango wa uuzaji wa hisa stahiki kwa Benki hiyo ikiwa ni kuongeza mtaji wa benki,uwekezaji na kuimarisha utoaji wa Mikopo nafuu kwa walimu,wafanyakazi na wafanyabiashara wa kati na wadogo.


Majaliwa amesema kwamba uuzaji wa hisa stahiki unatoa fursa kwa wanahisa kuongeza umiliki wao huku benki ikiimarisha uwezo wake wa kifedha.


Amesema kupitia mpango huo,MCB itaongeza mtaji,kupanua huduma kwa wananchi wengi zaidi,kuimarisha utoaji wa mikopo nafuu kwa walimu, wafanyakazi na wafanyabiashara wa kati na wadogo,pamoja na kuendeleza teknolojia za kidigitali.

"Ni fursa ya kifedha pekee, bali ni nafasi ya kuchangia ukuaji wa benki na maendeleo ya uchumi wa taifa,” amesema Majaliwa, huku akiwahimiza wanahisa kushiriki kikamilifu katika ununuzi wa hisa hizo.


Hata hivyo mpango huo unasimamiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), huku utekelezaji wake ukiongozwa na iTrust Finance Limited.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya MCB, Francis Ramadhani,amesema wanahisa wote waliokuwa kwenye rejesta kufikia Mei 5, 2026 wanastahili kununua hisa mpya tatu kwa kila hisa moja waliyonayo, kwa bei ya punguzo ya TSh 110.


Ameongeza kuwa dirisha la ununuzi wa hisa hizo tayari limefunguliwa, ambapo wanahisa wanaweza kununua hisa hizo kidigitali kupitia DSE Hisa Kiganjani,ofisi za Chama cha Walimu (CWT), pamoja na matawi ya benki hiyo.


"Mpango mpango huu umepata idhini ya Benki Kuu (BOT) na unatekelezwa kwa uwazi chini ya usimamizi wa CMSA na DSE,naomba niwasisitize wanahisa wote kushiriki ili kuimarisha mtaji wa benki na kukidhi matakwa ya kisheria."amesema Ramadhan.


Nae Mkurugenzi Mkuu wa MCB, Richard Makungwa, amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita benki hiyo imeonyesha ukuaji mkubwa wa kifedha.


Amesema mali za benki zimeongezeka kutoka chini ya TSh. bilioni 30 mwaka 2019 hadi TSh. bilioni 98 mwaka 2025, huku amana za wateja zikikua kutoka TSh. bilioni 16 hadi zaidi ya TSh.bilioni 75 katika kipindi hicho.

Powered by Blogger.