ZAIDI YAMABASI YA MWENDOKASI 150 YAPAKI, MOFAT CHANGAMOTO UKOSEFU WA ENEO LA HUDUMA
Na Mwandishi wetu
Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP-CENTRE) kimeeleza kuwa kampuni ya mabasi yaendayo haraka ya Mofat inakabiliwa na changamoto ya kukosa maeneo ya kutoa huduma, hali iliyosababisha zaidi ya mabasi 150 kubaki yamepaki tangu kununuliwa, huku mabasi 50 pekee yakiwa yanaendelea kutoa huduma ya usafiri wa abiria.
Akizungumza Mei 6, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa PPP-CENTRE, David Kafulila, alisema hali hiyo imeathiri uwekezaji wa mradi huo ambao una miezi sita tangu uanze kutekelezwa.
Kafulila alitoa kauli hiyo baada ya kufanya ziara ya kukagua mradi wa mabasi yaendayo haraka unaoendeshwa kwa ubia kati ya DART na kampuni ya Mofat, kwa lengo la kutathmini utekelezaji wake na kubaini changamoto zilizopo.
Alisema, kwa mujibu wa sheria, miradi ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi inapaswa kufuatiliwa na Serikali kuanzia hatua za awali hadi mwisho wake ili kuhakikisha uwekezaji unakuwa endelevu.
“Tumefanya ziara hii pamoja na wadau wa sekta binafsi ili kuona namna mradi huu unavyoendeshwa na kubaini changamoto zake. Tumegundua kuwa zaidi ya mabasi 150 yamekaa bila kutoa huduma kwa zaidi ya nusu mwaka, jambo linalosababisha hasara kwa mwekezaji,” alisema Kafulila.
Alishauri kampuni hiyo kuandaa ripoti ya tathmini ya utekelezaji wa mradi kwa kipindi cha miezi sita, ambayo itawasilishwa Serikalini kupitia kamati za juu za usimamizi wa miradi ya ubia ili kusaidia kufanyiwa maboresho na kutatua changamoto zilizopo.
Kwa upande wake, Msemaji wa kampuni ya Mofat, Philip Changala, alisema mradi huo ni wa kimkakati kwa manufaa ya Watanzania, hasa kwa wakazi wa Dar es salaam maeneo ya Mbagala, Kivukoni na Gerezani.
Alieleza kuwa ziara ya PPP-CENTRE imekuwa chachu kwa kampuni hiyo, kwani imeonesha dhamira ya Serikali ya kusikiliza na kutatua changamoto za wawekezaji binafsi ili kuboresha mazingira ya biashara.
Aidha, Changala alibainisha kuwa TPSF imekuwa na mchango mkubwa katika kuwasilisha changamoto za sekta binafsi Serikalini na kusaidia kupatikana kwa mrejesho.
“Tunatambua kuwa mahitaji ya usafiri ni makubwa na yanatofautiana kwa wananchi. Tunaendelea kubuni huduma mbalimbali ili kuwafikia watu wengi zaidi na kuhakikisha kila mmoja ananufaika na huduma zetu,” alisema Changala.t


