POLISI WACHUNGUZA KIFO CHA MWANAMKE ALIYEKUTWA DARAJA LA SALENDER
Na Mwandishi wetu-- Dar es salaam
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linaendelea kuchunguza taarifa ya kifo cha mwanamke aliyefahamika kwa jina la Aisha Miraji, ambaye mwili wake ulikutwa kwenye maji katika eneo la daraja la Salender, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, mwili huo ulikutwa Mei 11, 2026 majira ya saa 4:30 asubuhi ukiwa hauna jeraha lolote lililoonekana kwa nje.
.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa marehemu alikuwa mkazi wa Nzasa, Temeke. Inaelezwa kuwa Mei 10, 2026 alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiwa pamoja na wazazi wake kutokana na changamoto za kiafya zilizokuwa zikimsumbua kwa nyakati tofauti ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa marehemu alipotea ghafla akiwa katika eneo la hospitali hiyo kabla ya mwili wake kuonekana siku iliyofuata katika eneo la daraja la Salender.
Aidha, wazazi wa marehemu wameeleza kuwa mtoto wao alikuwa akikabiliwa na changamoto mbalimbali za kiafya kwa muda mrefu
Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini mazingira halisi ya kifo hicho.

