RAIS RUTO AITAMBUA TANZANIA KUWA KITOVU CHA NISHATI AFRIKA MASHARIKI

 




📌 Asisitiza ushirikiano wa kikanda kupitia miradi ya umeme na kiwanda cha kusafisha mafuta


Na Mwandishi Wetu


Rais wa Kenya, Mhe. William Ruto, amesema kuwa Tanzania ina nafasi ya kipekee ya kuwa kitovu cha nishati katika ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na uwekezaji mkubwa katika miradi ya kimkakati ya nishati.


Akilihutubia Bunge la Tanzania kwa mwaliko wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Mei 5, 2026, Rais Ruto alieleza kuwa miradi ya pamoja ya nishati kati ya Tanzania na Kenya inaendelea kuleta mapinduzi ya kiuchumi pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.


Alitaja mafanikio ya mradi wa umeme wa Kenya–Tanzania Power Interconnector wa msongo wa kilovolti 400, unaohusisha njia ya usafirishaji umeme yenye urefu wa zaidi ya kilomita 500.


Rais Ruto alisema mradi huo haujaunganisha tu gridi za umeme za nchi hizo mbili, bali pia umesawazisha mifumo ya umeme, kuwezesha biashara ya umeme, kuongeza upatikanaji wa nishati na kupunguza changamoto ya kukatika kwa umeme.


Aidha, alibainisha kuwa mipango ya mradi mpya wa kuunganisha umeme kupitia njia ya Shinyanga–Mabuki–Kilgoris–Rongai utaongeza uwezo wa usafirishaji wa umeme na kuimarisha soko la pamoja la nishati katika ukanda huo.


Alisisitiza kuwa ushirikiano huo utasaidia kutumia vyema rasilimali za nishati zilizopo Afrika Mashariki, ikiwemo gesi asilia ya Tanzania, nishati ya jotoardhi pamoja na vyanzo vingine vya nishati jadidifu, hatua itakayochochea ushindani na uhakika wa nishati.


Katika hatua nyingine, Rais Ruto alipongeza uamuzi wa Uganda kuwekeza katika kampuni ya ujenzi wa bomba la mafuta la Kenya, akisema hatua hiyo imeifanya nchi hiyo kuwa mshirika kamili badala ya kuwa mtumiaji tu wa miundombinu hiyo.


Pia alieleza kuwa Kenya iko tayari kuwa mshirika wa kimkakati katika mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta (refinery) mkoani Tanga. Alisema licha ya awali kutamani mradi huo ujengwe Mombasa, kijiografia Tanga ina faida ya ukaribu na Kenya hivyo kuwa eneo sahihi kwa utekelezaji wa mradi huo.


Rais Ruto alihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendelea kuwekeza katika miradi ya pamoja ya kimkakati ikiwemo mabomba ya mafuta na miundombinu ya nishati, ili kuimarisha usalama wa nishati na kukuza uchumi wa ukanda huo.

Powered by Blogger.