SERIKALI YAWEKEZA KUMALIZA SARATANI YA MACHO KWA WATOTO NCHINI
Serikali imeendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya ya macho kwa watoto hapa nchini kwa kutoa miongozo ya kitaifa ya utambuzi na matibabu ya saratani ya macho pamoja na mwongozo wa afya ya msingi ya macho kwa lengo la kuwawezesha wataalamu wa afya kutambua mapema wagonjwa na kuwapatia rufaa kwa wakati.
Hayo yamesemwa leo tarehe 15 Mei, 2026 jijini Dodoma katika Hospitali ya Rufaa ya Benjamin Mkapa na Dkt. Eliud Eliakim aliyemwakilisha Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe katika maadhimisho ya kitaifa ya wiki ya kuongeza uelewa kuhusu Saratani ya macho kwa watoto "Retinoblastoma" yaliyoanza tarehe 10 Mei, 2026.
"Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa miaka mitano wenye thamani ya shilingi bilioni 4.8 unaolenga kupunguza vifo na ulemavu wa macho kwa watoto katika mikoa ya Singida, Tabora, Arusha na Manyara katika awamu ya kwanza. Mradi huu unatarajiwa kuongeza uwezo wa huduma za uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya macho kwa watoto na kuimarisha kinga dhidi ya upofu unaozuilika," amesema Dkt. Eliud.
Aidha, amesema takwimu za kimataifa zinaonesha kuwa kati ya kila vizazi hai 16,000 hadi 18,000, mtoto mmoja uzaliwa akiwa na Saratani ya Retina, amesisitiza ugonjwa unatibika iwapo utagunduliwa mapema na mtoto kufikishwa kwenye huduma za afya kwa wakati. takwimu za utoaji huduma za afya nchini, zinaonesha kuwa watoto 902 waliougua saratani ya macho walihudumiwa katika vituo mbalimbali vya afya mwaka 2025, ikilinganishwa na watoto 184 waliopata huduma mwaka 2024.
Dkt. Eliud akihitimisha hotuba ya Mganga Mkuu wa Serikali ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuimarisha huduma za afya ya macho kwa watoto ili kuhakikisha watoto wote wanaohitaji huduma hizi wanazipata kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya Dkt. Hamad Nyembea amesema jumla ya Watoto 2,599,314 wenye umri wa chini ya miaka mitano (5) walionwa katika kliniki za kawaida za ngazi ya msingi, kati yao, watoto 290,960 walikuwa na shida ya macho ambapo miongoni mwao, asilimia 39 ni wenye matatizo ya macho yasiyo ya kuambukiza ikiwepo majeraha kwenye macho.
Ameongeza kuwa,ongezeko la magonjwa ya macho yasiyoambukiza yanahitaji uwekezaji mkubwa ili kufikia mahitaji hayo,ameeleza Serikali inaendelea kushirikiana na wadau katika kuhahikisha watoto wanafikiwa mapema na huduma za macho za kibingwa na kibingwa bobezi ikiwemo kuimarisha mifumo ya rufaa.

