WATAALAM WATAAMUA KIWANDA CHA MAFUTA KIJENGWE WAPI ''DANGOTE''


 

Bilionea na mfanyabiashara wa Afrika Aliko Dangote amekutana na rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan na kuahidi kwamba kiwanda cha kusafishia mafuta kitajengwa mwaka huu.

Dangote amesema kwamba kamati ya Wataalamu itatoa ushauri wao kuhusu ni eneo gani kiwanda hicho kitajengwa katika eneo la Afrika mashariki.

Awali rais wa Kenya William Samoei Ruto alikuwa amependekeza ujenzi wa kiwanda hicho kufanyika katika mji wa Tanga, lakini Dangote akasema angependelea ujenzi huo kufanyika mjini Mombasa.

Hatahivyo akizungumza hii leo baada ya kukutana na rais Samia , bwana Dangote amesema kwamba kuna masuala mengi ya kuzingatiwa kabla ya uamuzi kuhusu ni wapi ujenzi wa kiwanda hicho utafanyika.

Tajiri huyo amesema kwamba kiwanda anachotaka kujenga kitakuwa na ukubwa wa kusafisha mapipa 650,000 ya mafuta kwa siku.

''Kama kule Nigeria, hatukujenga kiwanda cha mafuta katika eneo lenye mafuta , tunajenga pale ambapo tunaweza kupata aina tofauti ya mafuta ghafi na kwamba kuna mambo mengi ambayo tunapaswa kuyafanyia utafiti'', alisema bilionea huyo.

Dangote amesema kwamba mataifa ya Afrika Mashariki yatamiliki kiwanda hicho bila kujali eneo kitakapojengwa.

Mkutano wa viongozi hao wawili unajiri kufuatia madai ya pendekezo la kujenga kiwanda cha kusafishia mafuta mjini Tanga Tanzania.

Powered by Blogger.