FIFA YAPIGA MARUFUKU VUVUZELA ZA MASHABIKI KATIKA KOMBE LA DUNIA 2026
Shirikisho la soka Duniani, FIFA, limetangaza kupiga marufuku matumizi ya Vuvuzela na filimbi ndani ya viwanja vyote vitakavyotumika katika kombe la Dunia 2026 nchini Marekani, Canada na Mexico.
Kwa mujibu wa kanuni mpya za viwanjani, Mashabiki watakaobainika na vifaa hivyo katika lango la kuingia watanyang’anywa au kuzuiwa kuingia uwanjani. Hatua hiyo inalenga kuboresha mazingira ya mechi kwa wachezaji, waamuzi, watazamaji na watangazaji.
Uamuzi huo unatarajiwa kuzua mjadala mkubwa hasa barani Afrika, ambapo vuvuzela ilijizolea umaarufu mkubwa wakati wa kombe la Dunia la mwaka 2010 nchini Afrika Kusini. Kwa wengi, vuvuzela ni sehemu ya utamaduni wa soka wa Afrika na huchangia hali ya shamrashamra viwanjani, huku wengine wakidai kelele zake huathiri mawasiliano ya wachezaji na ubora wa matangazo ya televisheni.
FIFA imesema marufuku hiyo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha usalama, uratibu na mazingira yenye udhibiti zaidi katika mashindano hayo yatakayoshirikisha timu 48 kwa mara ya kwanza katika historia ya kombe la Dunia.
Kombe la Dunia 2026 linatarajiwa kuanza Juni 11, huku mamilioni ya mashabiki kutoka sehemu mbalimbali za dunia wakihudhuria mashindano hayo makubwa ya soka.

