HORMUZ YAPAISHA TENA BEI YA MAFUTA DUNIA NJIA PANDA







Kuvunjika kwa mazungumzo ya Marekani na Iran kwafuta matumaini ya kushuka kwa bei za nishati duniani*


DAR ES SALAAM.

Dunia inazidi kushuhudia  kipindi kigumu cha sintofahamu ya nishati baada ya bei za mafuta kuanza kupanda kwa mara nyingine kufuatia kusimama kwa mazungumzo kati ya Marekani na Iran yaliyokuwa yameanza kutoa matumaini ya kurejea kwa utulivu katika Mlango wa Hormuz.


Siku chache zilizopita, masoko ya mafuta duniani yalikuwa yameanza kuonyesha dalili za kutulia ambapo bei za mafuta zilishuka kwa zaidi ya asilimia 6 hadi 7 baada ya taarifa za uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano na kufunguliwa kwa Hormuz, njia muhimu inayobeba karibu asilimia 20 ya mafuta yote yanayouzwa duniani.


Reuters, CNN, Al Jazeera na vyombo vingine vya kimataifa viliripoti kuwa wafanyabiashara wa mafuta walikuwa wameanza kuondoa kile kinachoitwa risk premium kutokana na matarajio ya amani kurejea katika Ghuba ya Uajemi.


Matumaini hayo sasa yanaonekana kuyeyuka.


Wiki hii Iran imetangaza kusitisha mawasiliano yasiyo ya moja kwa moja na Marekani huku ikitoa onyo jipya kuhusu hatima ya Hormuz, hatua iliyozua hofu mpya katika masoko ya nishati duniani.

Matokeo yake, bei ya mafuta ya Brent imeanza kupanda tena na kukaribia dola 98 kwa pipa, huku baadhi ya wachambuzi wakionya kuwa endapo hali itaendelea kuwa mbaya zaidi, mafuta yanaweza kurejea haraka katika viwango vya zaidi ya dola 100 kwa pipa.


*SIKU 94 ZA MGOGORO WA HORMUZ*


Taarifa zinaonyesha kuwa hadi sasa zimefika  takribani siku 94 tangu mgogoro wa Hormuz ulipoanza mwishoni mwa Februari mwaka huu.


Katika kipindi hicho, dunia imekumbwa na kile kinachoelezwa na wachambuzi wa nishati kuwa moja ya mishtuko mikubwa zaidi kuwahi kutokea katika historia ya soko la mafuta duniani.

Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa kiwango cha mafuta kinachopita Hormuz bado kiko chini sana ya kiwango cha kawaida ambapo kabla ya mgogoro huo wastani wa mapipa zaidi ya milioni 13 ya mafuta kwa siku yalikuwa yanapita katika njia hiyo ambapo  Mwezi Mei kiwango hicho kilishuka hadi karibu mapipa milioni 1.2 kwa siku pekee.


Kadhalika, hata ongezeko la mafuta kutoka Marekani halijaweza kuziba pengo hilo ambapo Reuters imeripoti kuwa Marekani imefikia rekodi ya kuuza nje mapipa milioni 5.6 kwa siku, lakini bado kiasi hicho hakitoshi kufidia upungufu uliosababishwa na Hormuz.


*DUBAI INALIA*


Kama kuna jambo ambalo limeishtua dunia, ni kuona hata nchi zinazozalisha mafuta kama Umoja wa falme za kiarabu (UAE) zikianza kuathirika ambapo bei za petroli za mwezi Juni zimeongezeka kwa asilimia 8 na kufikia kiwango cha juu zaidi katika karibu miaka minne. 

Bei ya Super 98 imefikia dirham 3.95 kwa lita, ikiwa ni karibu asilimia 50 juu kuliko ilivyokuwa mwezi Februari kabla ya mgogoro kuanza hii ikiwa  ina maana kuwa hata nchi yenye utajiri mkubwa wa mafuta haiwezi kujikinga dhidi ya athari za kuvurugika kwa njia kuu ya usafirishaji wa mafuta duniani.


*ULAYA NAYO IMEBANWA*


Barani Ulaya, athari zimeanza kuonekana katika gharama za usafiri, uzalishaji wa viwandani na maisha ya kila siku ambapo ripoti za taasisi za uchumi za Ulaya zinaonyesha kuwa endapo bei za nishati zitaendelea kuwa juu hadi mwisho wa mwaka huu, ukuaji wa uchumi wa baadhi ya mataifa makubwa ya Ulaya unaweza kushuka zaidi huku mfumuko wa bei ukiendelea kuwa tatizo.


Italia, Ugiriki, Uturuki na mataifa mengine ya Ulaya yameongeza uagizaji wa mafuta kutoka Marekani ili kukabiliana na upungufu uliotokana na mgogoro wa Hormuz.


*TATIZO SI MAFUTA TU*


CNN na Al Jazeera zimekuwa zikisisitiza kuwa maumivu ya Hormuz hayaishii kwenye mafuta ya magari pekee zikieleza kuwa njia hiyo pia ni muhimu kwa usafirishaji wa gesi asilia, mbolea na bidhaa nyingine za kimkakati. 


Taarifa zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 30 ya biashara ya mbolea aina ya urea duniani inahusishwa na nchi za Ghuba zinazotumia njia hiyo,  hivyo gharama za mbolea, uzalishaji wa chakula na usafirishaji wa mizigo nazo zimeanza kuathirika.

Hii ina maana kuwa kwa wakulima, viwanda na watumiaji wa kawaida duniani, athari za Hormuz sasa zinaonekana katika kila hatua ya mnyororo wa uchumi.


*DUNIA NJIA PANDA*


Leo dunia ipo katika njia panda.


Upande mmoja kuna matumaini kwamba mazungumzo kati ya Marekani na Iran yanaweza kurejea na kufungua mlango wa kurejesha shughuli za kawaida Hormuz huku upande mwingine kukiwa na  hofu kwamba kuvunjika kwa mazungumzo hayo kunaweza kuisukuma dunia katika awamu mpya ya kupanda kwa bei za mafuta, chakula, mbolea na huduma za usafiri.


Ndani ya siku 94 za mgogoro huu, imethibitika kuwa Hormuz si njia ya mafuta pekee ni mshipa wa uchumi wa dunia na kila unapoziba, dunia nzima hupata maumivu.

                 

Powered by Blogger.