WAWILI JELA MAISHA KWA KUUZA DAWA ZA KULEVYA
Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi imewahukumu kifungo cha maisha gerezani Suleiman Thabit Ngulangwa na Farid Hamis Said baada ya kuwakuta na hatia ya kosa la kujihusisha na dawa za kulevya aina ya heroin.
Katika hukumu iliyotolewa jana Juni 1, 2026, Jaji S.E. Kisanya amesema ushahidi wa upande wa mashtaka ulithibitisha pasipo shaka kuwa washtakiwa hao walikuwa wanamiliki wa dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 15.19.
Kwa mujibu wa Mchambuzi wa Serikali wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Leonida Daniel Michael amethibitisha mahakamani kuwa pakiti 16 zilizokamatwa katika umiliki wa washtakiwa hapo zilikuwa na dawa za kulevya aina ya heroin na zilikuwa na uzito wa kilo 15.19 baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kisayansi.
Sambamba na hilo mahakama hiyo ilibaini kuwa utetezi wa washtakiwa hao haukuweza kuibua shaka dhidi ya ushahidi wa mashahidi na vielelezo vilivyowasilishwa.
Katika hatua nyingine mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo Sharifa Selemani Bakari ameachiliwa huru baada ya mahakama ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha ushiriki wake katika kosa hilo.
Mbali na kifungo hicho, mahakama imeagiza heroin yote iliyokamatwa pamoja na vifaa vya kufungashia kuteketezwa kwa mujibu wa sheria.

