MBUNGE ANNE KILANGO AONGOZA MAPOKEZI YA SHUJAA WA AFCON U -17 SAME MASHARIKI


Mamia ya wananchi wa Kata ya Kalemawe, Kijiji cha karamba wilayani Same, wamejitokeza kwa wingi kumpokea nyumbani kwao nyota chipukizi wa soka, Issa Chole, ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya vijana ya Serengeti Boys chini ya umri wa miaka 17.


Mapokezi hayo yaliongozwa na Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki, Anne Kilango, pamoja na viongozi mbalimbali wa eneo hilo na wananchi waliokusanyika kumpongeza kijana huyo kwa kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya AFCON 2026 kwa vijana chini ya miaka 17.


Shangwe na nderemo zilitawala katika kijiji hicho huku wananchi wakionesha fahari yao kwa mafanikio ya Issa Chole, ambaye ameibuka kuwa mmoja wa vijana wanaolipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa kupitia mchezo wa soka.




Akizungumza katika hafla hiyo, Anne Kilango alisema mafanikio ya Issa Chole ni jambo kubwa kwa wakazi wa Same Mashariki na Taifa kwa ujumla kwani yanaonesha kuwa vijana wa eneo hilo wana uwezo wa kufikia ndoto zao wanapopewa fursa sahihi.


Alisema ujio wa mchezaji huyo nyumbani ni heshima kubwa kwa jimbo hilo na ushahidi kwamba uwekezaji katika michezo unaweza kuzaa matokeo chanya kwa vijana na jamii kwa ujumla.


Kilango alibainisha kuwa Issa Chole ni miongoni mwa vijana waliopitia mashindano ya Samia Cup, yanayoandaliwa kila mwaka katika Jimbo la Same Mashariki kwa lengo la kuibua na kukuza vipaji vya michezo.


Kwa mujibu wa mbunge huyo, zaidi ya timu 91 kutoka maeneo mbalimbali ya jimbo hilo hushiriki mashindano hayo, ambayo yamekuwa jukwaa muhimu la kuwapa vijana nafasi ya kuonesha uwezo wao.



Alisema kupitia mashindano hayo, vijana wengi wameanza kuonekana katika ngazi za juu za soka na wengine wamepata nafasi ya kujiendeleza katika taaluma ya michezo.


“Leo tunashuhudia matunda ya Samia Cup. Issa ametufanya tujivunie kama wananchi wa Same Mashariki na kama Watanzania. Hii ni ishara kwamba tuna vijana wengi wenye vipaji ambao wanahitaji kuungwa mkono,” alisema Kilango.


Aliongeza kuwa ataendelea kuimarisha mashindano hayo ili kuhakikisha vipaji zaidi vinaibuliwa na kupata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa.


Mbunge huyo pia aliahidi kuanzisha na kuendeleza michezo mingine ikiwemo mpira wa miguu kwa wasichana na mpira wa pete, kwa lengo la kuwapa vijana na watoto wa kike fursa zaidi za kukuza vipaji na kujenga ajira kupitia michezo.


Kwa upande wake, Issa Chole aliwashukuru wananchi wa Kalemawe pamoja na Anne Kilango kwa mapokezi makubwa aliyoyapata, akisema hakuwahi kutarajia kupokelewa kwa namna hiyo baada ya kurejea kutoka majukumu ya timu ya taifa.


Alisema mafanikio yake yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mashindano ya Samia Cup yaliyompa nafasi ya kuonekana na kuanza safari yake ya soka la ushindani, huku akiwataka vijana wengine kushiriki mashindano hayo kwa nidhamu, kujituma na kuwa na malengo makubwa maishani.


Baba mzazi wa mchezaji huyo, Mzee Musa Chole, alisema anajivunia maendeleo ya mwanawe katika soka na kusisitiza kuwa nidhamu, mazoezi na kujituma ndiyo msingi wa mafanikio katika mchezo huo.Aidha, alimuomba Mbunge Anne Kilango kuendelea kuunga mkono vijana kupitia Samia Cup ili vipaji zaidi viweze kuibuliwa na kuendelezwa.




Naye mmoja wa wananchi wa Kata ya Kalemawe alisema jitihada za mbunge huyo katika kuendeleza michezo zimekuwa na manufaa makubwa kwa vijana, kwani zimewapa hamasa ya kujituma, kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya, ulevi na vitendo vingine vinavyoweza kuharibu maisha yao, huku akimpongeza kwa kujitokeza kushiriki mapokezi hayo ambayo yameonesha mshikamano mkubwa kati ya viongozi na wananchi.

Powered by Blogger.