POLISI: WAHAMASISHAJI WA UVUNJIFU WA AMANI KABLA YA JULAI 7 MWAKA HUU WATAFUATILIWA KWA KARIBU.

 



Na Mwandishi wetu-Dodoma


Polisi imesema inaendelea kufuatilia kwa karibu shughuli za watu hao ambao wanaotumia mitandao ya kijamii ambapo  wamekuwa wakihamasisha maandamano yaliyopangwa kufanyika Julai 7 mwaka huu



Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi kwa saa 24 pamoja na ufuatiliaji wa mitandao ya kijamii umebaini kuwa baadhi ya watu hao wameondoka kwenye ajenda ya kuhamasisha maandamano yasiyozingatia matakwa ya sheria na sasa wameanza kuhamasisha vitendo vya kihalifu.


Katika taarifa iliyotolewa  Msemaji WA Jeshi la Polisi David Misime Juni 19, 2026, amesema licha ya kuwepo kwa hali nzuri ya usalama, bado kuna matukio machache ya kihalifu yanayojitokeza katika maeneo mbalimbali nchini, huku wahusika wake wakichukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria.


Jeshi hilo limefafanua kuwa katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na maswali kutoka kwa wananchi kuhusu hatua zinazochukuliwa dhidi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuhamasisha vitendo vya uvunjifu wa amani.


 Misime ameeleza kuwa miongoni mwa vitendo vinavyohamasishwa ni kufunga barabara, kuchoma moto shule ili kuzua taharuki kwa wazazi na walimu, kushambulia wananchi, kukata watu vichwa, kuua watu, pamoja na kuharibu mali za umma na binafsi.


Aidha, imebainika kuwa baadhi yao wanatumia majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kijamii kuhamasisha kuvamiwa kwa askari wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa lengo la kupora silaha na kuzitumia kutekeleza vitendo vya uhalifu.


Jeshi la Polisi limesisitiza kuwa uhamasishaji wa vitendo hivyo ni kinyume cha sheria za nchi, misingi ya utawala wa sheria pamoja na mikataba ya kikanda na kimataifa, na kwamba hali hiyo ni tishio kwa usalama wa taifa.


“Hakuna haki ya kuhamasisha kufanyika kwa vitendo vya kihalifu vinavyohatarisha maisha ya watu na mali zao, wala vinavyokiuka haki za wananchi wengine kwa kuwanyima uhuru wa kufanya shughuli zao za kila siku,”


 

Jeshi la Polisi limeongeza kuwa linaendelea kuchukua hatua stahiki dhidi ya watu wote wanaojihusisha na vitendo hivyo na kwamba wahusika watachukuliwa hatua kali za kisheria mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi.


Vilevile, limewataka wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kwa kutoa taarifa za watu wanaohamasisha au kupanga vitendo vya uhalifu, badala ya kusambaza ujumbe huo katika mitandao ya kijamii.


Polisi imewahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama nchini itaendelea kuwa tulivu, huku ikisisitiza kuwa amani, utulivu na usalama vitaendelea kulindwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya Jeshi la Polisi, vyombo vingine vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi wenyewe.

Powered by Blogger.